LAGOS, Nigeria
NIGERIA itafanya Uchaguzi Mkuu wake mwaka 2027, huku suala la usalama likiendelea kuwa ‘pasua kichwa’ katika maeneo mengi ya Taifa hilo.
Pia, utawala wa Rais Bola Ahmed Tinubu unakabiliwa na maswali magumu juu ya utawala bora, uwajibikaji na mustakabali wa demokrasia ya Nigeria.
Miaka mitatu ya muhula wa kwanza wa Rais Tinubu imegubikwa na matukio ya uhalifu wa vikundi vya kigaidi, hali ngumu ya maisha kwa wananchi, sambamba na kashfa za rushwa.
Mchambuzi wa siasa mjini Lagos, Ayodele Adio, anaamini Serikali iliyoko madarakani imeshindwa kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.
“Labda hawana uwezo, hawakujipanga au wanakosa watu sahihi wa kuongoza mashirika na wizara,” amesema Adio.
JARIBIO LA KUPINDUA SERIKALI
Katika suala la usalama, hivi karibuni watumishi waandamizi sita wa vyombo vya dola, wakiwamo wastaafu, walifunguliwa mashitaka ya uhaini, wakitajwa kusuka mpango wa kuipindua Serikali ya Rais Tinubu.
Mamlaka zinaeleza kuwa hayo ni mashitaka makubwa zaidi ya uhaini tangu Nigeria iliporejea katika utawala wa raia mwaka 1999.
MABADILIKO KUIOKOA SERIKALI?
Hivi karibuni, Rais Tinubu alifanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kwa kutengua uteuzi wa Waziri wa Fedha, pia akiahidi kuchukua hatua zaidi katika nafasi zingine.
Mabadiliko hayo yana maana gani? Adio anasema: “Ni msimu wa siasa. Rais anatumia mabadiliko hayo kama njia ya kutuma ujumbe kwa wananchi, kwamba anasikia vilio vyao.”
Hata hivyo, kwa Wanigeria walio wengi, mabadiliko hayo ni ya kisiasa, badala ya Serikali kujikita katika changamoto za msingi – ugumu wa maisha na kuzorota kwa hali ya usalama kunakoathiri shughuli za kibiashara.
“Hawa wanasiasa wanajifikiria wao tu, siyo kuwatazama wananchi,” anasema Afisa Ugavi mkazi wa Lagos, Okonkwo David.
Kwa upande wake, mfanyabiashara Isaac Okafor anasema gharama za bidhaa muhimu zimeendelea kupanda na kusababisha wananchi kushindwa kumudu.
Okafor anagusia pia suala la usalama, akisema: “Hali ni mbaya zaidi katika maeneo ya vijijini, ambako vurugu (zinazofanywa na waasi) zimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku.”


