Na mwandishi wetu, Gazetini
MATUKIO ya vyombo vya dola kuvibana mbavu vyombo vya habari yameshika kasi nchini Ethiopia kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Juni, mwakani.
Wengi watakumbuka kuwa Ethiopia iliingia katika machafuko ya vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2022, ambapo watu 600,000 walipoteza maisha na wengine milioni tano kuyakimbia makazi.
Kuhusu hali mbaya ya vyombo vya habari kuelekea Uchaguzi ujao, tukio lililozua mjadala mkubwa zaidi ni kupotea kwa mwandishi wa kituo cha redio cha Ahadu, Abdulsemed Mohamed. Hajaonekana tangu Agosti 11.
Akihojiwa, mkewe aitwaye Emebet Buta anaeleza kushangazwa na ukimya wa vyombo vya dola juu ya tukio hilo. “Polisi hawajatupa majibu, wamesema tu wataunda timu ya kumtafuta.”
Ukiweka kando kupotea kwa mtangazaji huyo wa vipindi vya biashara, mhariri wa Gazeti la Reporter, Yonas Amare, alivamiwa na kutekwa na watu walioficha sura zao. Ni tukio la siku mbili tu baada ya lile la Abdulsemed.
Mwaka 2023, Serikali ilivifungia vituo vya runinga vya kigeni 15, pia ikipandisha kwa kiasi kikubwa gharama za usajili.
Kwa mwaka jana pekee, waandishi sita walitupwa gerezani. Miongoni mwao ni Yeshihasab Abere aliyeachiwa Januari, mwaka huu.
“Machi, mwaka huu, waandishi sita wa vyombo vya habari binafsi wa Ethiopia walirejea uraiani wakitokea gerezani,” inaeleza ripoti ya Kamati ya Kuwalinda Waandishi (CPJ).
Katika mashitaka yanayowakabili, waandishi wanashutumiwa kuunga mkono vitendo vya ugaidi na kusambaza taarifa za chuki dhidi ya Serikali.
Kutokana na mfululizo wa matukio ya aina hiyo, mwanachama wa Taasisi ya Kimataifa ya Waandishi Wasio na Mipaka (RSF), Sadibou Marong, anasema kwa sasa maisha ya waandishi nchini Ethiopia yako hatarini kuliko kipindi chochote.
“Kukamatwa na kushikiliwa kwa waandishi wa habari kunaonesha ni kwa namna gani mamlaka za Ethiopia ziko mbali na jitihada za kuimarisha uhuru wao,” anasema Sadibou.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa waandishi, Taifa hilo la Afrika Mashariki lenye watu milioni 130, linashika nafasi ya 145 kati ya mataifa 180 kwenye viwango vya uhuru wa habari vya RSF.
Kwa upande mwingine, hali hiyo inakinzana na ahadi ya Waziri Mkuu, Abiy Ahmed, ambaye wakati anaingia madarakani mwaka 2018 aliahidi kurejesha mazingira mazuri ya utendaji kwa waandishi wa habari.
Kinyume chake, akiwa Ufaransa mwezi uliopita, Abiy aliliomba Taifa hilo kumsaidia kuwakamata waandishi wa Ethiopia wanaokosoa uongozi wake wakiwa nchini humo.
Inaelezwa kuwa Serikali ya Ethiopia imefanya jitihada hizo za kudhibiti waandishi wake walioko katika mataifa ya Ulaya, Afrika Kusini, Kenya na Uganda.
Published:


