Na Mwandishi Wetu, Gazetini-Dar es Salaam
BENKI ya NCBA imezindua rasmi kampeni yake mpya ya kibiashara inayojulikana kama “Numbers That Matter- Maisha Ni Hesabu”, ikiwa ni ishara ya kujidhatiti upya katika kuchochea maendeleo na athari chanya kwa jamii ya Tanzania.
Kampeni hiyo inalenga kuonyesha namna kila uamuzi-kuanzia chaguo la kifedha hadi hatua za kijamii—unavyoweza kupelekea maendeleo yenye maana kwa mtu mmoja mmoja, biashara na taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NCBA Bank, Alex Mziray, amesema kampeni hiyo inaakisi dhamira ya benki hiyo ya kwenda mbali zaidi ya huduma za kifedha za kawaida.
“Kwa NCBA, tunataka namba ziwe simulizi za maendeleo ya familia, biashara na taifa. ‘Maisha Ni Hesabu’ siyo tu kuhusu miamala, bali ni kipimo cha athari halisi katika maisha ya watu,” amesema Mziray.
Kupitia kampeni hiyo, NCBA imeonesha mchango wake katika ukuaji wa sekta muhimu ikiwemo bidhaa za viwandani (FMCG), usafirishaji na mawasiliano, mafuta na gesi, pamoja na viwanda. Huduma zake za kifedha zilizolengwa zimewezesha wateja kupanua biashara, kuongeza mauzo na kujenga ushindani.
“Wateja wetu wanapokua, sekta nzima inakua. Huo ndio nguvu ya ‘hesabu zenye maana’,” aliongeza Mziray.

Katika sekta ya umma, biashara na utalii, benki hiyo imekuwa kinara wa mikakati inayojenga uthabiti huku ikipunguza athari kwa mazingira. Kupitia ajenda hiyo ya maendeleo endelevu, NCBA imeahidi kupanda zaidi ya miti 10,000 nchini Tanzania ifikapo 2025. Tayari miti 5,000 imepandwa kando ya Mto Mpiji, Bunju B, ikiwa ni juhudi za kudhibiti mmomonyoko wa udongo na kurejesha ubora wa maji.
Benki hiyo pia inaendelea kuwekeza katika watu na jamii kupitia Mashindano ya Gofu ya NCBA, yanayohamasisha wachezaji chipukizi na wanawake huku yakiwa jukwaa la viongozi wa kibiashara na mabalozi wa mabadiliko kukutana.
“Nafasi yetu ni kufungua milango-iwe ni kwenye biashara, michezo au utunzaji wa mazingira. Kupitia mikutano hii, tunathibitisha kuwa ukuaji ni shirikishi,” alisema Mziray.
NCBA imethibitisha uimara wake wa kifedha baada ya kupata ongezeko la asilimia 24 ya faida kabla ya kodi mwaka 2024, ikifikia Sh bilioni 16.1 ikilinganishwa na Sh bilioni 13.0 mwaka 2023. Ukuaji huo umetokana na kuaminika kwa wateja pamoja na bidhaa bunifu kama NCBA Now App na huduma za mikopo ya mali.
Akihitimisha hotuba yake, Mziray ameongeza kuwa; “Ahadi yetu ya chapa ni rahisi-Go For It. Kupitia kampeni hii, tunawaonyesha Watanzania kwamba kila namba, kila hatua na kila uamuzi ni sehemu ya kujenga kesho tunayoitaka sote.”


