9.5 C
New York

Kutembea haraka hupunguza vifo vya mapema

Published:

LONDON, Uingereza

KUTEMBEA haraka, walau kwa dakika 15 tu kila siku, huimarisha afya ya moyo na kuepusha vifo vya mapema kwa asilimia 19, utafiti umebaini. Utafiti huo umefanywa nchini Marekani na kuhusisha watu zaidi ya 79,850 kutoka katika familia za kipato cha kati.

Majibu yake yameonesha kuwa kutembea haraka kwa dakika 15 ni bora zaidi kuliko mwendo wa taratibu utakaotumia saa tatu (dakika 180).

Wataalamu kupitia utafiti huo wanashauri kuwa walau hatua 14 za miguu kwa dakika moja kinaweza kuwa kipimo sahihi cha utembeaji wa haraka.

Utafiti umekuja baada ya takwimu zilizoonesha kuwa vifo vya ghafla vitokanavyo na magonjwa ya moyo vimeongezeka kwa kasi katika kipindi kifupi cha miaka 10 ya hivi karibuni.

Kwa Uingereza pekee, watu 420 hufariki kila wiki kutokana na magonjwa ya moyo, idadi ikifikia 21,975 kwa mwaka.

Wakati huo huo, kundi la vijana wenye umri wa miaka 25-29 limeonekana kuwa hatarini zaidi, idadi ya vifo ikiongezekana kwa asilimia 95.

Akizungumzia utafiti huo, Profesa Wei Zeng anasema njia hiyo huimarisha ufanisi wa utendaji-kazi wa moyo na kupunguza unene uliopitiliza.

“Mfumo wa maisha ni tatizo kubwa. Mtu atatoka nyumbani na kuingia kwenye gari au treni akienda kazini. Akifika, anakaa kwa muda mrefu. Akiwa anarudi, pia anakaa kwenye gari au treni. Akifika nyumbani, anakaa kuangalia runinga.

“Kampeni na programu za afya zinapaswa kusisitiza umuhimu wa kutembea haraka ili kupunguza tatizo (la vifo vya haraka),” anasema Prof. Zeng.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img