Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Amos Makalla amejata majina ya wagombea sita wa Jimbo Bumbuli mkoani Tanga ambapo aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kipindi kilichopita Januari Makamba jina lake halijapita.
Makalla ametaja orodha ya majina ya wateule wa jimbo hilo watakaokwenda kupigiwa kura za maoni leo Julai 29, 2025, jijini Dodoma, ambao ni Hidaya Kilima, Zahoro Rashid Hanuna, Eng. Ramadhan Singano, Rashid Salimu, Silas Joram na John Aloyce.

Naye aliyekuwa Mbunge wa Kisesa mkoani Simiyu, Luhaga Mpina ameshindwa kupenya katika watiania saba wa ubunge wa jimbo hilo waliopitishwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuingia katika mchakato wa kura za maoni ambapo waliopita ni Lusingi Makanda, Silinde Mhachile, Joel Mboyi, Madili Sakumi, Godfrey Mbuga, Elias Mambembela na Gambamala Luchuga.
Aidha aliyekuwa kada wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Ester Matiko, amepenya katika katika kinyang’anyiro cha kura za maoni, Jimbo la Tarime Mjini mkoani Mara akiwa miongoni mwa wagombea sita walioteuliwa.


