9.5 C
New York

JET, IUCN wawanoa waandishi wa habari kuhusu uchumi wa buluu

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini-Tanga

Katika kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanakuwa mstari wa mbele kuelimisha jamii na kuchochea sera kuhusu uchumi wa buluu, Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Uasilia (IUCN) kupitia Mradi wa Bahari Mali, wameendesha warsha ya mafunzo maalum kwa wanahabari 15 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Akifungua rasmi warsha hiyo siku mbili ya iliyofanyika jijini Tanga mapema leo Julai 23, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, amesema kuna haja ya waandishi kupewa maarifa ya kina kuhusu masuala ya bahari ili wawe mabingwa wa masuala ya uchumi wa buluu na kuisaidia jamii kuelewa fursa na changamoto zilizopo.

Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.

“Huu ni wakati muafaka kwa waandishi wa habari kujifunza juu ya masuala ya bahari na uchumi wa buluu ili waweze kuwa wabobevu katika eneo hili muhimu kwa kukuza uchumi wa nchi,” amesema Chikomo.

Ameongeza kuwa matarajio ya JET ni kuona waandishi wanaandika kwa weledi na kuibua mijadala kuhusu uchumi wa buluu, ili kuongeza uelewa wa jamii na pia kuhamasisha utekelezaji wa sera rafiki za kulinda mazingira ya baharini.

Kwa upande wake, Meneja wa Programu wa IUCN Tanzania, Joseph Olila, amesema Tanzania bado haijaitumia ipasavyo fursa ya uchumi wa buluu licha ya kuwa na eneo kubwa la bahari.

“Hili ni eneo lenye fursa nyingi lakini hatujalifanyia kazi ipasavyo. Tunaamini nyie waandishi ni kundi sahihi la kufikisha maarifa haya kwa jamii na kusaidia kuchochea mabadiliko. Vyombo vya habari vinapaswa kuwekeza nguvu zaidi katika eneo hili,” amesema Olila.

Meneja wa Programu wa IUCN Tanzania, Joseph Olila.

Mradi wa Bahari Mali unaotekelezwa na IUCN unalenga kuimarisha maisha ya jamii za pwani, kulinda ikolojia ya baharini na kukuza ustahimilivu wa tabianchi. Sehemu muhimu ya mradi ni kuongeza uelewa wa umma na kushawishi sera kupitia mawasiliano yenye athari chanya.

Katika warsha hiyo, Dk. Blandina Lugendo amesisitiza umuhimu wa kulinda nyasibahari kama sehemu ya mifumo ya ikolojia ya baharini, akieleza kuwa dhana ya upandaji wa nyasi bahari ni mpya nchini na ilianza kutekelezwa mwaka 2018.

“Nchi kama Kenya na Msumbiji tayari zimeanza hatua ya urejeshwaji wa nyasibahari. Sisi pia tunapaswa kuchukua hatua ili kulinda mazingira yetu ya baharini kwa ustawi wa uchumi wa buluu,” amesema Dk. Blandina.

Kupitia warsha hiyo, waandishi hao wanatarajiwa kuwa mabalozi wa uchumi wa buluu nchini, wakiibua mijadala yenye tija, kushawishi mabadiliko ya sera, na kusaidia jamii kufahamu namna bora ya kunufaika na rasilimali za baharini kwa njia endelevu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img