LONDON, England
KITENDO cha mshambuliaji wa Brentford, Yoane Wissa, kuondoka katika kambi ya timu hiyo huko Ureno kimeibua tetesi kuwa huenda amerejea London kukamilisha usajili wake wa kujiunga na Tottenham.
Wissa mwenye umri wa miaka 28, amekuwa akihusishwa na Tottenham kwa wiki kadhaa, pia akitajwa kuwindwa na Newcastle, Tottenham na Nottingham Forest.
Taarifa zinaeleza kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ameshakubaliana masilahi binafsi na Tottenham.
Brentford wamejaribu kumshawishi asaini mkataba mpya lakini Wissa ameonesha nia ya kuondoka klabuni hapo majira haya ya kiangazi.
Endapo ataondoka, atakuwa mchezaji wa pili kuipa kisogo Brentford baada ya Bryan Mbeumo kujiunga na Manchester United kwa Pauni milioni 65.
Wissa alijunga na Brentford mwaka 2021 akitokea Lorient ya Ligue 1 na ameshaifungia timu hiyo jumla ya mabao 49 katika michezo 149.
Msimu uliopita, aliingia kambani mara 19 katika mechi 35 za Ligi Kuu ya England (EPL).
Published:


