LONDON, England
KIUNGO wa zamani wa Chelsea, John Obi Mikel, ameitaka klabu hiyo kusajili mlinda mlango mpya kama inataka kutwaa mataji msimu ujao.
Chelsea imetanua kikosi chake majira haya ya kiangazi kwa kuwasajili Liam Delap, Joao Pedro na Jamie Gittens.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Obi, bado kocha Enzo Maresca anapaswa kurudi sokoni na kusajili kipa.
Kwa sasa, lango la Blues linawategemea Robert Sanchez na Filip Jorgensen, ambao hata hivyo hawakuonesha viwango bora msimu uliopita.
Obi raia wa Nigeria, alitwaa mataji mawili ya Ligi Kuu ya England kwa misimu 11 aliyocheza Stamford Bridge. “Mashabiki wengi wa Chelsea wanaweza kukubaliana na mimi, kwamba tunahitaji kipa wa viwango vya juu kwa sababu Sanchez hatoshi,” alisema Obi katika mahojiano yake na mtandao wa talkSPORT.
“Suala la kipa mpya linapaswa kufanyiwa kazi. Hatuwezi kwenda msimu mpya tukiwa na Sanchez.”
Katika siku za hivi karibuni, Chelsea wamekuwa wakihusishwa na mlinda mlango wa PSG na timu ya taifa ya Italia, Gianluigi Donnarumma.
Ukiacha Donnarumma atakayemaliza mkataba wake na PSG mwakani, pia Chelsea wanamtolea macho Mike Maignan wa AC Milan.
Published:


