13.9 C
New York

Dembele; ndoa ilivyookoa kipaji kilichozikwa na majeraha, kamari

Published:

PARIS, Ufaransa

KWA rahisi, maisha yake ndani ya klabu ya Barcelona yalitawaliwa na vurugu nyingi lugha za ndani na nje ya uwanja. Baada ya kucheza kwa kiwango cha juu akiwa na klabu za Rennes na Borussia Dortmund, Ousmane Dembele alijikuta akiishi maisha magumu Camp Nou.

Kama itakumbukwa, ni hapo ndipo alipojikuta akitumia siku 784 nje ya uwanja kutokana na majeraha 14 ya nyama za paja.

MAISHA YA KAMARI

Alipotua Barca mwaka 2017 akitokea Dortmund, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa pili kusajiliwa kwa fedha nyingi duniani. Hata hivyo, licha ya thamani yake kubwa sokoni, maisha yake ya nje ya uwanja nayo yalitawaliwa na vurugu nyingi.

Kama si matukio ya kurudi usiku mwingi kutokana na tabia yake ya kucheza kamari katika klabu za starehe, basi ni Dembele kuchelewa mazoezini.

Mwenendo huo ulisababisha kugombana mara kwa mara na mabosi wa Barca na hata kumfanya kuwa mchezaji anayeongoza kwa kutozwa faini kutokana na matukio ya utovu wa nidhamu.

AMEZALIWA UPYA

Tangu alipojiunga na PSG, Dembele mwenye umri wa miaka 28 amekuwa kwenye kiwango bora na msimu huu ameshaingia kambani mara 35 na kutoa ‘asisti’ 16 katika mechi 53.

Mchango wake huo wa mabao umeiwezesha timu yake kutwaa mataji ya Ligi ya Mabingwa, Ligi Kuu (Ligue 1) na Kombe la Ligi (Coupe de France). Takwimu hizo zinamfanya Dembele kuwa kipaumbele cha wengi katika kinyang’anyiro cha tuzo ya Ballon d’Or ya mwaka huu.

NDOA IMEMSAIDIA ‘KUTOBOA’

Kwa upande mwingine, inaaminika kuwa siri ya kiwango bora alichonacho sasa ni ndoa yake na mrembo aitwaye Rima. Iko hivi; wawili hao walifunga ndoa mwaka 2021 nchini Morocco. Ni baada ya hapo, ndipo Dembele alipoelekea kwao, Ufaransa, na kuajiri mtaalamu wa saikolojia.

Vilevile, kama hiyo haitoshi, Dembele alizama mfukoni na kuajiri mtaalamu wa masuala ya lishe, ambaye pia anatokea Ufaransa. Ikumbukwe, miaka miwili tu baada ya ndoa, Dembele aliondoka Barca na kujiunga na PSG kwa ada ya Pauni milioni 44.

MBAPPE AMPA BALLON D’OR

Mwezi uliopita, Mfaransa mwenzake anayekipiga Real Madrid, Kylian Mbappe, aliweka wazi kuwa Dembele ndiye mchezaji wake bora kwa sasa. Mbappe ambaye pia aliwahi kuwika akiwa na matajiri wa Ligue 1, PSG, alisema hayo alipoulizwa juu ya mchezaji anayeweza kumpigia kura katika kinyang’anyiro cha Ballon d’Or.

“Nitampigia kura Dembele? Ndiyo. Sidhani kama hilo linahitaji maelezo zaidi. Watu wa nazungumzia Lamine Yamal na Dembele, lakini chaguo langu liko wazi. Nitampigia kura Dembele,” alisema Mbappe.

Pia, mshambuliaji wa zamani wa Tottenham, Real Madrid na timu ya taifa ya Wales, Gareth Bale, naye anaamini tuzo ya mwaka huu ya Ballon d’Or itatua mikononi mwa Dembele.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img