15.5 C
New York

Mastaa wa kuchungwa WAFCON 2025

Published:

BERKANE, Morocco
FAINALI za Mataifa Afrika kwa soka la Wanawake zilianza kutimua vumbi Julai 5, mwaka huu, zikifanyika kwa msimu wa pili mfululizo nchini Morocco.
Je, ni Afrika Kusini tena safari hii, kama walivyonyakua ubingwa msimu uliopita wa mashindano hayo ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF)?
Kwa upande mwingine, safari hii kuna vita ya wachezaji wanaofanya vizuri katika soka la wanawake.
Asisat Oshoala (Nigeria)
Oshoala (30), aliiongoza Nigeria kufika hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia mwaka 2023 na sasa anafukuzia taji lake la nne la WAFCON.
Nyota huyo wa Bay FC ya Ligi Kuu ya Marekani (NWSL) ameibeba mara sita tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa CAF.
Pia, ni mshindi mara mbili wa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Barcelona.
Clara Luvanga (Tanzania)
Luvanga alifunga ‘hat-trick’ mbili wakati timu yake ya Al-Nassr ilipotwaa taji la Ligi Kuu ya Saudi Arabia msimu uliopita.
Kwa ujumla, alimaliza msimu akiwa ameingia kambani mara 19, akimaliza nafasi ya nne katika chati ya wafungaji bora.
Straika huyo mwenye umri wa miaka 20, amebeba mara mbili ubingwa wa michuano hiyo akiwa na Al-Nassr.
Sanaa Mssoudy (Morocco)
Mssoudy alikuwa tegemeo kikosini wakati timu yake ya AS FAR ilipomaliza msimu na kubeba taji la Ligi Kuu ya Morocco bila kupoteza mchezo.
Kutokana na makali yake, mshambuliaji huyo ndiye aliyeibuka Mchezaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.
Kama hiyo haitoshi, Mssoudy mwenye umri wa miaka 25 akawa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Morocco.
Jermaine Seoposenwe (Afrika Kusini)
Anakipiga Ligi Kuu ya Mexico akiwa na vigogo wa soka la nchi hiyo, Monterrey.
Seoposenwe (31), ndiye tegemeo kwa sasa baada ya mfungaji bora wa WAFCON ya mwaka 2018, Thembi Kgatlana, kujitoa kikosini kutokana na sababu binafsi.
Nyota huyo ameshacheza mechi zaidi ya 100 tangu alipoanza kuitumikia Banyana Banyana mwaka 2010.
Kama alivyoeleza hivi karibuni, Seoposenwe atastaafu kandanda mara tu zitakapomalizika fainali hizi.
Aissata Traore (Mali)
Traore alifunga mabao manne katika safari ya Mali kufuzu fainali hizi za WAFCON. Mali haikuwa imekata tiketi tangu mwaka 2018.
Traore (27), alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Ufaransa msimu uliopita akiwa na kikosi cha Fleury 91.
Katika kikosi cha Mali, Traore anashirikiana na staa wa PSG, Agueicha Diarra, kuunda ‘pacha’ hatari ya ushambuliaji.
Barbra Banda (Zambia)
Mshambuliaji wa Orlando Pride ya Marekani, ambaye tayari ameshaingia kambani mara nane msimu huu.
Kwa mabao yake 10, Banda ndiye Mwafrika (kwa soka la wanawake na hata wanaume) aliyefunga mara nyingi katika historia ya Olimpiki.
Wakati huo huo, Banda mwenye umri wa miaka 25 ndiye anayeishikilia tuzo ya Mchezaji Bora wa CAF.
Pia, Banda anashika nafasi ya pili katika orodha ya wachezaji wa soka la wanawake wenye thamani kubwa zaidi kuwahi kutokea Afrika.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img