Na Mwandishi Wetu, Gazetini
BAADA ya taarifa nyingi zinazomtaja kiungo Stephane Aziz Ki kurudi Yanga, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, amefunguka. Aziz Ki, akiwa mmoja ya wachezaji tegemeo kikosini, aliondoka Yanga miezi michache iliyopita na kujiunga na vigogo wa soka la Morocco, Wydad Casablanca.
Kwa siku za hivi, hasa baada ya nyota huyo kuonekana kushindwa kujihakikishia namba katika kikosi cha kwanza cha Wydad, zimekuwapo tetesi za kurejea kwake Jangwani. Sasa, kwa mujibu wa Ofisa Habari, Kamwe, mkataba wa Yanga na Wydad unaitaka klabu hiyo ya Morocco kumtumia Aziz Ki kwa miezi mitatu.
“Endapo ndani ya hiyo miezi mitatu wakiona wanataka kuendelea naye, basi watamsainisha mkataba wa miaka miwili na kuongeza kiasi cha pesa ambacho kipo ndani ya huo mkataba.
“Uongezaji wa mkataba ni lazima ufanyike kabla ya tarehe 10 Julai 2025. Ifahamike bado sisi kama Yanga tuna mkataba na Aziz Ki wa mwaka mmoja. “Endapo Wydad wakiona hawawezi kuendelea naye, basi atarudi kambini kuendelea na kazi yake hapa Jangwani,” amesema Kamwe.


