Na Mwandishi wetu
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Pindi Chana amesema asali ya Tanzania imeuzwa nje ya nchi kwa kiwango kikubwa kwa thamani ya sh 15.85 bilioni kwa mwaka 2024 ikilinganishwa na sh 5.16 bilioni zilizouzwa nje ya nchi hapo awali.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2025/2026 bungeni jijini Dodoma leo Mei 19, 2025 Dk. Chana amesema thamani ya mazao ya misitu na nyuki imezidi kuimarika.
Amesema katika kuhakikisha jamii inaendelea kushiriki kwenye uhifadhi na uendelezaji wa rasilimali za misitu na nyuki, wizara hiyo imekamilisha maandalizi ya Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Ufugaji Nyuki kwa Tanzania Iliyo Bora.

Waziri huyo amesema mpango huo unalenga kuongeza kiwango cha uzalishaji wa asali kutoka tani 33,861 za sasa hadi kufikia tani 75,000 ifikapo Juni, 2035 na kuongeza mauzo ya mazao ya nyuki katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Aidha, mpango huo unatarajiwa kuongeza ajira mpya 43,055 kupitia shughuli zilizopo katika mnyororo wa thamani wa ufugaji nyuki.
Ameeleza kuwa sambamba na hilo, Wizara imeandaa na kusaini Hati ya Makubaliano ya usimamizi wa mradi wa ufugaji nyuki kati ya Wizara, WAGA WMA na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.

“Kwa lengo la kuongeza wigo wa biashara ya asali, kwa niaba ya Serikali Wizara imesaini Itifaki kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China inayoruhusu uuzaji wa Asali ya Tanzania nchini China.
“Utiaji saini wa Itifaki hii umefungua milango kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuuza asali inayozalishwa nchini katika soko la nchini China,”amesema Waziri Chana.
Aidha amesema Shirika la Wafugaji Nyuki Duniani limeiteua Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa wafugaji nyuki duniani mwaka 2027 ambapo mkutano huo utahudhuriwa na wadau zaidi ya 4,000 kutoka sehemu mbalimbali za dunia.


