Na Ramadhan Hassan,Dodoma
Wizara ya Ujenzi imetaja vipaombele 10 vya mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2025-2026 ikiwemo kuendelea na ujenzi wa barabara za kimkakati zenye kufungua fursa za kiuchumi, kuimarisha shughuli za kijamii pamoja na zile zinazounganisha barabara na njia nyingine za usafiri.
Vipaumbele hivyo vimetajwa leo bungeni Mei 5,2025 na Waziri wa Ujenzi,Abdallah Ulega wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2025-2026 ambapo Wizara hiyo inaomba kuidhinishiwa zaidi ya Sh trilioni 2.28.
Waziri Ulega amevitaja vipaombele hivyo kuwa ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa barabara zinazounganisha makao makuu ya mikoa, nchi jirani pamoja na barabara za ulinzi kwa kiwango cha lami, kuendelea na ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano katika miji inayokua kwa kasi na majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Morogoro;
Pia, kuendelea na ukarabati na matengenezo ya barabara kuu na mikoa ili kuhakikisha kuwa barabara zinapitika katika majira yote ya mwaka pamoja na matengenezo makubwa ili kuhakikisha kuwa barabara haziendelei kuharibika na kupoteza thamani.
Vipaumbele vingine ni kuimarisha usafiri na miundombinu ya vivuko ili kuunganisha maeneo ya nchi kavu ambayo yametenganishwa na maji katika maeneo ya bahari, maziwa na mito;
Vilevile, kuendeleza na miradi ya usalama barabarani ikiwemo kujenga mizani pamoja na kusanifu na kujenga barabara za michepuo na zile zinazozingatia mahitaji ya watumiaji wote wa barabara.
Pia, kujenga nyumba za watumishi wa umma na majengo ya Serikali kwa kuupa kipaumbele utaratibu wa kushirikisha sekta binafsi,kuwajengea uwezo wataalam wa ndani kwa lengo la kuongeza wataalam wabobezi wa ndani, pamoja na kutoa kipaumbele kwa kampuni za ndani zinazohusika na masuala ya ujenzi;
Vipaumbele vingine ni mapitio ya Sera, miongozo na mifumo inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi ili iendane na wakati ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya teknolojia na maendeleo na kukamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege vilivyokasimiwa wizara hiyo , ikiwamo Msalato.


