Na Ramadhan Hassan,Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeishauri Serikali kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi yake yote ili iweze kuakisi viwango bora, uendelevu na kuwepo kwa thamani ya fedha.
Ushauri huo umetolewa leo bungeni na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Ally Mlaghila wakati akiwasilisha maoni ya kamati hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Mjumbe huyo wa kamati akiwasilisha kwa niaba ya Mwenyekiti wa kamati hiyo,Moshi Kakoso, imeipongeza Serikali kwa ufanisi wa kuendelea kutoa fedha za kutekeleza majukumu mbalimbali ya Fungu 98 – Wizara ya Ujenzi, hususan katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema kwa muktadha huo, kwa kuthamini mtaji wa fedha za maendeleo unaotokana na kodi za wananchi, Kamati inaishauri kuongeza ufanisi na ubunifu katika utendaji kazi utakaochochea kuboresha huduma za Sekta ya Ujenzi nchini kutokana na umuhimu sekta.
Pia kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi yake yote ili iweze kuakisi viwango bora, uendelevu na kuwepo kwa thamani ya fedha.
Vilevile kuongeza ufanisi na ubunifu katika kukusanya maduhuli kutokana na vyanzo vilivyopo, na kubaini vyanzo vipya ambavyo vitaongeza wigo wa makusanyo hayo.
Amesema sambamba na hilo, Serikali ihakikishe huduma zitolewazo na taasisi zake, zinakuwa bora ili kukidhi matarajio ya wadau muhimu wa Sekta ya Ujenzi.


