MADRID, Hispania
TANGU alipoajiriwa kuchukua mikoba ya Carlo Ancelotti majira ya kiangazi, mwaka huu, kocha Xabi Alonso amekuwa akitajwa kuingia kwenye uhusiano mbaya na staa wa klabu hiyo raia wa Brazil, Vinicius.
Hiyo imesababisha kuwapo kwa taarifa nyingi zinazomuhusisha mshambuliaji huyo na mpango wa kufungasha virago vyake na kuondoka Santiago Bernabeu.
Hata hivyo, Vinicius si wa kwanza kukorofishana na kocha huyo, ambaye pia aliwahi kuitumikia Madrid akiwa mchezaji.
Jude Bellingham
Kwa mujibu wa kile kilichoripotiwa na Gazeti la Mundo Deportivo la Hispania, staa mwingine wa Madrid, Bellingham, naye hana uhusiano mzuri na Alonso.
Licha ya kucheza asilimia 46 pekee ya mechi za msimu huu wa La Liga na kufunga mabao sita katika mechi sita, nyota huyo raia wa England hafurahii maisha chini ya kocha huyo.
Rodrygo
Akiwa ameingia mara tatu pekee kikosi cha kwanza msimu huu wa La Liga, haishangazi kuona Mbrazil huyo akimchukia Alonso.
Taarifa kutoka Brazil zinasema haelewani na Alonso na ndiyo sababu ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 kutaka kuondoka Madrid wakati wa usajili uliopita wa majira ya kiangazi.
Endrick
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 19 amecheza dakika 11 pekee za La Liga tangu Alonso alipoanza majukumu ya kuliongoza benchi la ufundi la Madrid.
Ripoti zilizopo zinaeleza kuwa nyota huyo anajiandaa kuondoka Santiago Bernabeu kupitia dirisha dogo la usajili wa Januari, mwakani, ambapo anahusishwa zaidi na Lyon ya Ufaransa.
Fede Valverde
Mwezi uliopita, ziliibuka taarifa kuwa kuna ‘bifu’ linaloendelea kati ya Alonso na nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay. Nyota huyo hafurahii nafasi anayochezeshwa.
Wakati Valverde mwenye umri wa miaka 24 akiwa anapenda zaidi kucheza eneo la kiungo, Alonso amekuwa akimtumia kama beki wa kulia.
Jonas Hofmann
Historia ya Alonso kutkorofishana na wachezaji wake haikuanzia Madrid. Hata akiwa na Bayern Leverkusen, hakuwa na mahusiano mazuri na nyota wa kikosi hicho, Hofmann.
Nyota huyo aliwahi kusema hakuwa akizungumza na Alonso, hasa katika msimu wa mwisho wa kocha huyo klabuni hapo.
Patrick Schick
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29, aliweka wazi kuwa msimu uliopita, kwamba angeondoka Bayern Leverkusen endapo Alonso angebaki klabuni hapo.
Schick alikasirishwa na kitendo cha kocha huyo kumsugulisha benchi, licha ya kwamba alikuwa na mchango mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji.
Published:


