27 C
New York

Kuelekea Kombe la Dunia 2026: Ivory Coast (42)

Published:

ABIDJAN, Ivory Coast
TAIFA hilo la Afrika ya Magharibi linashika nafasi ya 42 katika viwango vya ubora wa soka duniani. Ivory Coast iliwahi kuwa ya 12 mwaka 2013.
‘The Elephants’ wana historia kubwa katika soka la Afrika. Ni mabingwa mara tatu wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON); 1995, 2015 na 2023.
Hata hivyo, kwa upande wa Kombe la Dunia, wamerejea baada ya kuikosa michuano hiyo tangu mwaka 2014. Itakuwa ni mara yao ya nne kushiriki mashindano hayo.
Kuelekea katika fainali zijazo za mwakani, Ivory Coast inanolewa na Emerse Fae, ambaye amekuwa kwenye benchi la ufundi tangu alipoajiriwa Januari, mwaka jana.
Fae ni mchezaji wa zamani wa Ivory Coast na alikuwa kikosini wakati timu hiyo ilipofuzu kwa mara ya kwanza mwaka 2006.
Katika michuano hiyo iliyofanyika nchini Ujerumani, waliishia hatua ya makundi, kama walivyofanya mwaka 2010 na 2014.
Aidha, Ivory Coast watakwenda kwenye michuano hiyo wakiwa na kikosi chenye nyota kadhaa wanaotamba na klabu mbalimbali za soka barani Ulaya.
Miongoni mwao ni Nicolas Pepe (Villarreal), Franck Kessie (Al Ahli) na Amad Diallo (Manchester United). Pia, wanaye Seko Fofana aliyefunga mabao matatu katika mechi za kufuzu.
Matumaini ya kuiona Ivory Coast ikifanya vizuri katika fainali za Kombe la Dunia za mwakani ni makubwa, hasa kwa namna walivyofuzu bila kuruhusu bao.

Related articles

Recent articles