TOKYO, Japan
NI moja ya timu zilizofuzu na itakuwa miongoni mwa zile 48 zitakazokwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia za mwakani.
Japan inashika nafasi ya 18 katika viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Hata hivyo, Taifa hilo la barani Asia liliwahi kusogea hadi nafasi ya tisa mwaka 1998. Jina la utani la timu ya soka ya taifa ya Japan ni ‘Samurai Blue’.
Japan ni mabingwa mara nne wa Kombe la Asia wakiwa wamefanya hivyo katika miaka ya 1992, 2000, 2004 na 2011.
Chini ya kocha mzawa, Hajime Moriyasu, ambaye amekuwa kwenye benchi tangu mwaka 2018, Japan ilikuwa timu ya kwanza kufuzu.
Moriyasu, ambaye huu ni mwaka wake wa saba kwenye benchi, aliiongoza Japan kufika fainali ya Kombe la Asia mwaka 2019, ambapo walifungwa mabao 3-1 na Qatar.
Kocha huyo ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo. Mwaka 1993, alikuwa mchezaji wakati Japan ilipokosa tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia baada ya kufungwa na Iraq.
Hii itakuwa mara yake ya pili akiwa kocha wa Japan kwenye fainali za Kombe la Dunia. Katika mechi 98 tangu aajiriwe, Moriyasu amefungwa 17 pekee na ana asilimia 67 ya ushindi.
Kikosi hicho kina wachezaji kadhaa wanaofanya vizuri barani Ulaya, wakiwamo Takumi Minamino (Monaco), Kaoru Mitoma (Brighton) na Ayase Ueda (Feyenoord), ambaye alifunga mabao saba katika mechi za kufuzu.
Wakati huo huo, kikosi cha Japan kinaye mshambuliaji aliyeng’ara msimu uliopita wa Kombe la Dunia (2022), Ritsu Doan.
Doan aliifungia Japan bao la kusawazisha katika mechi mbili ngumu dhidi ya Ujerumani na Hispania, ambazo zote zilipomalizika kwa Japan kupata ushindi wa mabao 2-1.
Nyota huyo anatarajiwa kufanya makubwa tena msimu ujao wa Kombe la Dunia kwani ameshahusika katika mabao matano ya mechi tano za Bundesliga akiwa na Frankfurt.
Hii ni mara ya nane mfululizo kwa Japan kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia lakini haijawahi kuvuka hatua ya mtoano (16 Bora).
Msimu uliopita wa fainali za mwaka 2022 nchini Qatar, licha ya kuifunga Hispania katika mchezo wa mwisho wa makundi, walitolewa na Croatia.
Published:


