LONDON, Uingereza
HIVI karibuni, jina la Raheem Sterling lilishika nafasi kubwa katika vyombo vya habari vya Uingereza na barani Ulaya kwa ujumla baada ya kuhukumiwa kifungo cha miezi 12 gerezani kwa kosa la uendeshaji wa gari wa hatari.
Mbali na hukumu hiyo, ametakiwa kutokuendesha gari kwa miaka miwili, sambamba na kutakiwa kufanya kazi ya kijamii isiyo na malipo kwa saa 100 [miezi zaidi ya mitatu].
Hukumu hiyo ilitokana na ajali aliyopata akiwa anaendesha gari lake la kifahari aina ya Lamborghini miezi kadhaa iliyopita.
Kwa upande mwingine, Sterling aliyezaliwa Kington, Jamaica, amekuwa na maisha yenye matukio tangu akiwa mdogo. Alipokuwa na umri wa miaka miwili tu, baba yake aliuawa kwa kupigwa risasi.
Baada ya kifo cha baba, mama yake Sterling, Nadine, alihamia na watoto wake Uingereza, wakati huo akisoma, pia akifanya kazi ya usafi wa vyoo na kubadili mashuka katika vyumba vya hoteli ili kupata fedha za kujikimu.
Wakiishi mjini Neasden, Kaskazini-Magharibi mwa London, Sterling alianza safari ya elimu katika Shule ya Vernon House, huku tabia ya ukorofi zilikuwa sehemu ya maisha yake.
Akihojiwa mwaka 2018, Sterling alisema: “Nilikuwa mtundu kiasi kwamba nilifukuzwa nikiwa shule ya msingi. Sikutaka kumsikiliza yeyote zaidi ya mama yangu. Hilo lilikuwa tatizo langu kubwa.”
Akiwa na umri wa miaka 10 tu, mwalimu wake, Chris Beschi, alimwambia: “Kama utaendelea na tabia hii uliyonayo, ukifikisha miaka 17 utakuwa mchezaji wa timu ya taifa ya England au utakuwa gerezani.”
Miaka ikapita na Sterling akaianza rasmi safari ya mafanikio ya soka akiwa na umri wa miaka 15 tu baada ya Liverpool kumsajili akitokea QPR mwaka 2010.
Alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na Liverpool miaka miwili baadaye na kisha kuwa mchezaji mdogo zaidi baada ya Michael Owen kuifungia bao timu hiyo. Aliandika historia hiyo akiwa na miaka 17.
Mwaka 2012, akiwa bado ana miaka 17, Sterling alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na ‘uzi’ wa England walipofungwa na Sweden mabao 4-2 mjini Stockholm.
Katika ubora wake, alitwaa mataji manne ya Ligi Kuu ya England akiwa na klabu tofauti za Liverpool, Chelsea, Arsenal na Manchester City na kufunga jumla ya mabao 123 na ‘asisti’ 65 katika mechi 396 za michuano hiyo.
Nje ya uwanja, Sterling, kama ilivyokuwa enzi za utoto, aligubikwa na matukio mengi, licha ya ustaa wake kwenye soka la England na Ulaya.
Akiwa na umri wa miaka 20 mwaka 2015, zilisambaa picha zikimuonesha Sterling akivuta shisha. Hiyo ilimkera kocha wake wakati huo pale Liverpool, Brendan Rodgers, ambaye alimuonya akimwambia atapotea kama asingeachana na mfumo huo wa maisha.
Haikuishia hapo. Sterling alizua tena gumzo wakati wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2018 zilizofanyika nchini Urusi.
Wakati huo akiwa na kikosi cha timu ya Taifa, England, ilisambaa picha ya ‘tattoo’ ya bunduki aina ya M16 aliyoichora kwenye mguu wake.
“Nikiwa na miaka miwili, baba yangu aliuawa kwa kupigwa bastola na niliahidi kuanzia hapo kwamba sitowahi kushika bastola katika maisha yangu,” alisema.
Kwa sasa, maisha yake ya soka yamesimama. Sterling hajacheza soka tangu alipoitumikia Feyenoord ya Ligi Kuu nchini Uholanzi katika mechi ya Mei 17, 2026. Alikamatwa na polisi siku 11 tu baada ya mchezo huo.


