10.6 C
New York

Magenge ya uhalifu yanavyoitesa Serikali ya Mexico – [6]

Published:

SINALOA, Mexico

KWA mujibu wa sheria za Mexico, raia wanaruhusiwa kumiliki silaha za moto, ingawa kuna umakini mkubwa wa Serikali katika kuzuia uholela wa manunuzi yake.

Hata hivyo, magenge ya uhalifu yamekuwa yakitumia zaidi bunduki na bastola aina ya AR-15, M16, M4, AK-47, AKM na Type 56, ambazo raia wa kawaida hawaeruhusiwa kumiliki.

Idara ya Kudhibiti Dawa za Kulevya ya Marekani (DEA) katika ripoti yake imeeleza kuwa vikundi vya kihalifu vilivyoko Mexico siku hizi vinatumia silaha za kisasa kuliko vile vya awali.

Lakini, watafiti na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mexico wanaeleza wazi kuwa sehemu kubwa ya silaha hizo hazizalishwi nchini humo, na badala yake zinatoka katika viwanda vya Marekani.

Hilo lilikuja kuthibika baadaye, ambapo mamlaka za Mexico zilikamata silaha takribani 30,000 kati ya mwaka 2004–2008 na 7,200 kati ya hizo, sawa na asilimia 87, zilitokea kwa majirani zao hao.

Takwimu zinaonesha hivyo, licha ya kwamba Marekani imekuwa bega kwa bega na mamlaka za Mexico katika kukabiliana na wimbi la magenge ya uhalifu kwa kuipatia teknolojia, vifaa, mafunzo na taarifa za kiusalama.

Kwa upande mwingine, kwa miaka mingi utitiri wa magenge ya uhalifu nchini Mexico umekuwa ukihusishwa moja kwa moja na kiwango cha kutisha cha umasikini kwa wananchi walio wengi. Kuanzia mwaka 2004 hadi 2008, kiwango cha watu masikini kiliongezeka kutoka asilimia 17 hadi asilimia 21.

Kuanzia mwaka 2006 hadi 2010, kiwango kiliongezeka mara dufu kutoka asilimia 35 hadi asilimia 46, huku Mexico ikiwa moja ya nchi za Kusini mwa Amerika zenye tofauti kubwa kati ya matajiri na masikini.

Kutokana na ugumu wa maisha, magenge ya uhalifu yamegeuka chanzo cha ajira. Mwaka 2012, ripoti moja ilieleza kuwa vikundi vya kihalifu vimezalisha ajira za moja kwa moja 450,000 na watu takribani milioni 3.2 wanaishi kwa kutegemea biashara ya ‘unga’.

Ripoti hiyo ilitolea mfano Mji wa Ciudad Juarez, ikieleza kuwa asilimia 60 ya uchumi wake unategemea vipato vinavyopatikana kwa njia zisizo halali.

Kwa takwimu za mwaka 2023, watu 175,000 nchini Mexico wanafanya kazi na magenge hayo. Sinaloa Cartel peke yake inatajwa kuwa na wanachama 45,000 katika nchi zaidi ya 100 duniani.

Achilia mbali umasikini, changamoto ya wananchi wengi kukosa elimu ncini Mexico nayo inatajwa kuwa faida kubwa kwa magenge ya uhalifu.

Ripoti ya Jukwaa la Uchumi Duniani [WEF] inaeleza kuwa Mexico inashika nafasi za chini [31] katika nchi 134 zinazowekeza vizuri kwenye sekta ya elimu.

Kama hiyo haitoshi, mfumo wake wa elimu ya msingi unashika nafasi ya 116 duniani. Mwaka 2011, waalimu katika Mkoa wa Acapulco walikabiliwa na matukio ya kutekwa na kuteswa, hali iliyosababisha wagome kufanya kazi.

Mwisho …

Related articles

Recent articles