20.3 C
New York

Ukiacha Messi, hawa nao wanakipiga Ligi Kuu ya Marekani

Published:

LONDON, Uingereza
KWA miaka mingi ya hivi karibuni, Ligi Kuu ya Marekani (MLS) imekuwa ikipokea wachezaji wenye majina makubwa kutoka katika klabu za barani Ulaya, hasa England.
Miongoni mwa mwa mastaa waliojiunga na MLS hivi karibuni ni Lionel Messi, Son Heung-min, Luis Suarez na Thomas Muller.
Hata hivyo, wapo wengine ambao huenda mashabiki wengi wa soka wangedhani kuwa walishastaafu. Bado wapo na wanakipiga MLS.
Marco Reus
Kiungo wa zamani wa Borussia Dortmund, Reus, alitua MLS mwaka jana akitokea Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga). Anayazungumziaje maisha mapya ndani ya Marekani?
“Kwa kweli, MLS siyo Ligi maarufu sana Ujerumani. Lakini, nafikiri Ligi hii ni kubwa. Ina wachezaji wengi wazuri, naziona mechi nyingi nzuri hapa,” anasema.
Katika mechi yake ya kwanza akiwa LA Galaxy, Mjerumani huyo alifunga bao na kutoa ‘asisti’. Tayari ana ma ao 21 katika mechi 39 alizocheza klabuni hapo.
Hugo Lloris
Mlinda mlango wa zamani wa Tottenham na timu ya taifa ya Ufaransa. Aliondoka klabuni hapo mwaka 2023, akiwa amehudumu kwa miaka 11, akicheza mechi 450.
Lloris alifungasha virago na kujiunga na Los Angeles FC baada ya kupoteza namba mbele ya Guglielmo Vicario, ambaye kocha Ange Postecoglou alionekana kumpa nafasi zaidi.
Kwa misimu miwili ya hivi karibuni, amekuwa chaguo la kwanza katika lango la LA FC. “Nilihitaji maisha mapya baada ya mafanikio makubwa nikiwa Ulaya,” anasema.
Wilfred Zaha
Winga aliyetwaa taji la Ligi Kuu ya Uturuki (Super Lig) msimu wa 2023-24 akiwa na vigogo wa soka nchini humo, Galatasaray.
Msimu uliopita, 2024-25, alikuwa Lyon kwa mkopo lakini aliishia kucheza dakika 71 pekee katika mechi za Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).
Kwa sasa, Zaha anaitumikia Charlotte ya MLS, ambapo ameshahusika katika mabao 16 akiwa amecheza mechi 35.
Christian Benteke
Baada ya kiwango kizuri akiwa na Aston Villa, mshambuliaji huyo alijiunga na Liverpool kwa ada ya Pauni milioni 32.5. Hiyo ilikuwa mwaka 2015.
Hata hivyo, kwa msimu mmoja aliocheza Anfield, Benteke alifunga mabao 10. Akarejea Crystal Palace kwa ada ya Pauni milioni 32.
Straika huyo alicheza kwa miaka sita Ligi Kuu ya England, kabla ya kujiunga na D.C United ya MLS. Mwaka jana, akawa mfungaji bora wa MLS kwa mabao 23 katika mechi 30.
Eric-Maxim Choupo-Moting
Alipowika na Stoke City mwaka 2018, Choupo-Moting alipata mafanikio makubwa kwa miaka sita aliyocheza PSG na Bayern Munich.
Nyota huyo raia wa Cameroon alitwaa mataji 10 kwa nyakati tofauti akiwa na klabu hizo za Ligue 1 na Bundesliga.
Kwa sasa, Choupo-Moting anakipiga New York Red Bulls ya MLS na ameshafunga mabao 18 katika mechi 38.
Hirving Lozano
Winga huyo aliwahi kuhusishwa na klabu za England, ikiwamo Chelsea, wakati huo akiwa na Napoli ya Serie A, hata alipokuwa PSV ya Ligi Kuu ya Uholanzi.
Lozano alitua San Diego FC mwanzoni mwa mwaka huu baada ya kusumbuliwa na majeraha katika msimu wake wa mwisho akiwa PSV.
Akiwa na umri wa miaka 30 kwa sasa, nyota huyo ameshafunga mabao 10 katika mechi 32 na anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Mexico kwenye fainali za Kombe la Dunia za mwakani.
Emil Forsberg
Baada ya miaka nane ya kuwika RB Leipzig ya Bundesliga, Forsberg alijiunga na New York Red Bulls mwaka jana na kuwa mchezaji anayelipwa mshahara mnono zaidi klabuni hapo.
Msimu wake wa kwanza, 2024-25, alihusika katika mabao 14 katika mechi 23. Msimu huu, raia huyo wa Sweden mwenye umri wa miaka 34 ameshazifumania nyavu mara 13.
Rob Holding
Alicheza mechi zaidi ya 160 akiwa na Washika Bunduki wa London, Arsenal. Aliondoka klabuni hapo mwaka jana na kutua Crystal Palace.
Hata hivyo, baada ya kushindwa kujihakikishia namba, Palace walimpeleka kwa mkopo Sheffield United, kabla ya kutua Colorado Rapids wakati wa usajili wa majira ya kiangazi, mwaka huu.

Related articles

Recent articles