LONDON, Uingereza
LICHA ya kwamba dirisha dogo halitafunguliwa hadi Januari, mwakani, kwa sasa klabu za soka barani Ulaya zinaruhusiwa kusajili wachezaji huru (waliomaliza mikataba).
Makala haya yanakuibulia wachezaji wenye majina makubwa, ambao hawana ajira baada ya kumaliza mikataba yao katika klabu walizokuwa wakizitumikia.
Rui Patricio
Mlinda mlango huyo aliwahi kuwika Ligi Kuu ya England (EPL) akiwa na kikosi cha Wolves. Patricio hana klabu tangu alipoachana na Al Ain.
Aliondoka katika klabu hiyo ya Falme za Kiarabu baada ya kuitumikia katika fainali za Kombe la Dunia kwa ngazi ya Klabu.
Patricio amekuwa akihusishwa na Ligi Kuu ya Italia (Serie A). Aliwahi kucheza huko mwaka jana akiwa na Atalanta.
Takehiro Tomiyasu
Beki wa kulia wa zamani wa Arsenal. Tomiyasu raia wa Japan alicheza mechi 84 akiwa na Washika Bunduki hao wa Kaskazini mwa London.
Kutokana na majeraha ya mara kwa mara, mlinzi huyo aliondoka Emirates akiwa amehudumu kwa miaka minne.
Tomiyasu ana umri wa miaka 27 na huenda akarudi kwenye soka la ushindani barani Ulaya baada ya kupona majeraha ya goti.
Alex Oxlade-Chamberlain
Kiungo wa kati huyo wa zamani wa timu ya taifa ya England, anaendelea kujifua na timu ya vijana wa U-21 ya Arsenal akiwa mchezaji huru.
Oxlade-Chamberlain hana klabu tangu alipovunja mkataba wake na vigogo wa Ligi Kuu ya Uturuki, Besiktas.
Nyota huyo amekiri kupokea ofa nyingi lakini ameweka wazi kuwa zinatoka nje ya England, wakati yeye akitamani zaidi kucheza nyumbani.
Mitalem Pjanic
Wakati fulani akiwa na vigogo wa soka la Italia, AS Roma, Pjanic aliwahi kuwa miongoni mwa viungo bora katika soka la Ulaya. Hana klabu kwa sasa.
Pjanic mwenye umri wa miaka 35, amekuwa nje ya soka la ushindani kwa miezi kadhaa, tangu alipoachana na CSKA Moscow ya Urusi.
Aliondoka klabuni hapo Juni, mwaka huu, na kwa sasa nyota huyo ana ofa nyingi tu kutoka Marekani na Saudi Arabia, pia zikiwapo chache za barani Ulaya.
Dele Alli
Kiungo mshambuliaji huyo mwenye asili ya Nigeria atakumbukwa kwa ubora wake wa misimu kadhaa iliyopita akiwa na Tottenham na timu ya taifa ya England.
Baada ya muda mfupi wa kuitumikia Como ya Ligi Kuu ya Italia, ambayo inanolewa na Cesc Fabregas, Alli anaingia kwenye orodha hii ya wachezaji huru kwa sasa.
Ofa nyingi za klabu zinazomtaka zinatoka Daraja la Kwanza, ambapo Wrexham, Birmingham na West Brom zinatajwa kuitaka saini yake.
Dimitri Payet
Aliwahi kuwika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) akiwa na Marseille. Pia, alitamba England akiitumikia klabu kongwe ya London, West Ham United.
Payet, raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 38, alisifika zaidi kwa uwezo wake wa kufunga mabao ya mipira ya kutenga.
Nyota huyo ni mchezaji huru kwa sasa baada ya kuachana na vigogo wa soka la Brazil, Vasco da Gama. Anaendelea kuuguza majeraha ya goti.
Lorenzo Insigne
Nyota huyo anayecheza eneo la kiungo wa pembeni amekuwa mchezaji huru tangu alipoondoka Toronto FC ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS) miezi mitano iliyopita.
Kwa siku za hivi karibuni, Insigne raia wa Italia anahusishwa zaidi na mpango wa kujiunga na Lazio ya Serie A.
Endapo dili hilo litakamilika, Insigne atakutana na kufanya kazi na kocha Maurizio Sarri, ambaye aliwahi kufanya naye kazi wakiwa Napoli.
Maro Balotelli
Mshambuliaji wa kati raia wa Italia, ambaye atakumbukwa kwa uwezo wake mkubwa, lakini pia kwa matukio yake ya utukutu akiwa ndani na nje ya uwanja.
Balotelli hana klabu kwa sasa. Amekuwa mchezaji huru tangu alipotemwa na Genoa ya Italia miezi kadhaa iliyopita.
Kwa siku za hivi karibuni, nyota huyo mwenye umri wa miaka 35 amekuwa akihusishwa na klabu za Ligi Kuu ya Marekani (MLS).
Published:


