Na Hassan Mwasha, Gazetini
MATAIFA tisa ya Afrika yameshajihakikishia tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia za mwakani zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico. Tunisia, Algeria, Ghana, Misri, Senegal, Afrika Kusini, Ivory Coast, Cape Verde na Morocco.
Makala haya yanawaangazia wawakilishi hao wa soka la Afrika kwa kuichambua Senegal. Je, ina nafasi ya kufanya vizuri Kombe la Dunia?
Senegal ‘Simba wa Teranga’ wanaelekea katika fainali za Kombe la Dunia baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Mauritania, mchezo uliochezwa mjini Dakar.
Nahodha wa kikosi, Sadio Mane, alifunga mawili na kufikisha mabao matano katika mechi za kuwania tiketi ya kucheza Kombe la Dunia, kabla ya Iliman Ndiaye na Idrissa Gana Gueye nao kuingia kambani.
Senegal walifuzu wakiwa kileleni mwa Kundi B baada ya kufikisha pointi 26, wakifunga mabao 22 na kuruhusu mara moja tu nyavu zao kutikiswa.
Ubora wa safu ya ulinzi unatokana na uwepo wa Kalidou Koulibaly, Moussa Niakhate na Edouard Mendy, ambao kwa pamoja waliweza kucheza mechi nane kati ya 10 bila kuruhusu bao.
Senegal wana historia ya kuvutia katika michuano hii ya Kombe la Dunia; ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya Ufaransa na hatimaye kufika robo fainali katika fainali zao za kwanza kushiriki mwaka 2002.
Katika fainali zilizofuata za mwaka 2018 nchini Urusi, chini ya kocha Aliou Cisse, ambaye alikuwa nahodha wa kikosi mwaka 2002, Senegal ilikosa kidogo tu kuingia hatua ya 16 bora.
Mwaka 2022, Senegal walirejea Kombe la Dunia wakiwa na Cisse kwenye benchi la ufundi. Safari hii, walivuka makundi na kuishia hatua ya 16 bora baada ya kufungwa mabao 3-0 na England ‘Three Lions’.
Kwa sasa, kikosi hicho kinanolewa na Pape Thiaw aliyekabidhiwa mikoba mwishoni mwa mwaka jana. Juni, mwaka huu, Senegal ilithibitisha kurejesha makali yake baada ya kuichapa England mabao 3-1 katika mchezo wa kirafiki.
Ikiwa ni mara yao ya nne kushiriki Kombe la Dunia, safari hii Senegal watakuwa na kiu ya kuingia nusu fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano hiyo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Published:


