10.9 C
New York

Afrika na safari ya Kombe la Dunia 2026 (6) – Cape Verde

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini
MATAIFA tisa ya Afrika yameshajihakikishia tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia za mwakani zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico. Tunisia, Algeria, Ghana, Misri, Senegal, Afrika Kusini, Ivory Coast, Cape Verde na Morocco.
Makala haya yanawaangazia wawakilishi hao wa soka la Afrika kwa kuichambua Cape Verde. Je, ina nafasi ya kufanya vizuri Kombe la Dunia?
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Cape Verde na soka la Afrika kwa ujumla, Kisiwa hicho chenye watu wasiofikia 600,000 kimefuzu kushiriki Kombe la Dunia.
Cape Verde, Taifa dogo zaidi kufuzu Kombe la Dunia, walikata tiketi Oktoba 13, mwaka huu, na ni baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Eswatini. Ni mchezo wao wa mwisho waliokuwa mbele ya mashabiki wao 8,000.
Matokeo hayo yaliifanya Cape Verde kukaa kileleni mwa Kundi D ikiwa na pointi 23. Katika mechi 10 za kufuzu, ilishinda saba, ilitoa sare mbili na kufungwa moja.
‘Blue Sharks’ wako chini ya kocha Pedro Brito ‘Bubista’, ambaye aliajiriwa mwaka 2020. Kwa misimu sita ya hivi karibuni, Bubista ameiongoza Cape Verde kushiriki AFCON mara nne. Kati ya hizo, wamefika robo fainali mara mbili.
Kikosi chake kinaundwa na wachezaji wanaocheza soka katika mataifa 14. Katika mechi dhidi ya Eswatini, kikosi cha kwanza hakikuwa na mchezaji wa Ligi ya ndani.
Kati ya mabao 16 ya timu hiyo katika safari ya kufuzu, manne yalifungwa na Dailon Rocha Livramento, mshambuliaji mwenye umri wa miaka 24 tu.
Je, baada ya kufanya vizuri katika soka la Afrika kwa miaa ya hivi karibuni, Cape Verde itamudu ushindani mkali uliopo Kombe la Dunia? Ina ubavu wa kuvuka hatua ya makundi katika msimu wake wa kwanza?
Historia inaweza kuwarudisha kwa Senegal, ambao licha ya ugeni wao katika fainali za mwaka 2002, bado waliweza kuishangaza dunia kwa kufika robo fainali ya mashindano hayo.
Hata Hivyo, kufuzu pekee inaweza kuwa hatua kubwa kwao. Kwamba Cape Verde itashiriki Kombe la Dunia ikiwa haina cha kupoteza na hiyo itawasaidia kuepuka presha.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img