Na mwandishi wetu, Gazetini – DAR
KUANZIA kwa Nelson Mandela wa Afrika Kusini, Hakainde Hichilema wa Zambia hadi Bassirou Diomaye Faye wa Senegal, wote waliwahi kutumikia kifungo gerezani, kabla ya kuwa marais katika nchi zao.
Hichilema, ambaye amewahi kuwa kiongozi wa upinzani nchini Zambia, alikamatwa na polisi Aprili, 2017, na kushtakiwa kwa kosa la uhaini. Msafara wake ulidaiwa kuzuia msafara wa Rais Edgar Lungu.
Hichilema alikanusha tuhuma hizo, huku mashirika ya haki za binadamu yakikosoa kukamatwa kwake na matumizi mabaya ya shtaka la uhaini.
Alikaa gerezani kwa takribani karibu miezi minne, kuanzia Aprili hadi Agosti, 2017, kabla ya mashitaka hayo ya uhaini kuondolewa na kuachiwa huru Agosti 16, 2017.
Hatimaye, Hichilema alimshinda Edgar Lungu katika uchaguzi wa 2021 na kuapishwa kuwa rais wa Zambia mnano Agosti 24, 2021. Alishinda tena hivi karibuni uchaguzi wa Urais na ameanza muhula wake wa pili.
Kwa upande wake, Bassirou Diomaye Faye, alisota gerezani kwa miezi 11 wakati huo akiwa kiongozi wa upinzani na Katibu Mkuu wa Chama cha PASTEF.
Alikamatwa Aprili, 2023, baada ya chapisho lake kwenye mitandao ya kijamii na akashitakiwa kwa makosa ya kusambaza taarifa za uongo na kudharau mahakama.
Faye alikamatwa Aprili 14, 2023, na kukaa gerezani hadi Machi, 2024, ikiwa ni takribani miezi 11. Baadaye, alishinda uchaguzi wa urais na kuapishwa kuwa Rais mwezi mmoja baadaye.
Kuhusu Alpha Conde, alikaa jela kwa miaka miwili akiwa mwanasiasa wa upinzani aliyekuwa akipinga utawala wa Rais Lansana Conte.
Baada ya uchaguzi wa urais wa mwaka 1998, Conde alikamatwa karibu na mpaka wa Côte d’Ivoire na kutuhumiwa kujaribu kuondoka nchini Guinea kinyume cha sheria, kupinga kukamatwa na kupanga kuipindua serikali.
Mwaka 2010, alishinda uchaguzi wa urais wa Guinea na kuingia madarakani Desemba, 2010. Alihudumu kwa miaka 11 [2010 hadi 2021], kisha kupinduliwa kijeshi.
Ukiacha hao, unakumbuka kuhusu Olusegun Obasanjo? Alidumu gerezani wka miaka mitatu na alishawahi kuwa kiongozi wa kijeshi wa Nigeria kabla ya kukamatwa mwaka 1995.
Serikali ya kijeshi ya Jenerali Sani Abacha ilimkamata baada ya kumtuhumu kuhusika katika njama ya mapinduzi. Alihukumiwa kifungo cha maisha, kifungo kilichopungua baadaye hadi miaka mitatu [1995 hadi 1998].
Aliachiliwa baada ya kifo cha Abacha mwaka 1998 na Obasanjo alishinda uchaguzi wa urais wa Nigeria mwaka 1999. Alihudumu kwa mihula miwili (miaka 8) kama rais.
Historia inatumbusha pia kuhusu Jacob Zuma aliyewahi kusota jela kwa miaka 10 akiwa mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi nchini kwake, Afrika Kusini.
Alikamatwa mwaka 1963 alipokuwa akijaribu kuondoka Afrika Kusini pamoja na wanachama wengine wa harakati hiyo. Alihukumiwa kifungo cha miaka miaka 10 [1963 hadi 1973].
Alianza kutumikia kifungo hicho akiwa na umri wa miaka 21 tu na baadaye alikuja kuwa rais wa Afrika Kusini mwaka 2009. Alihudumu kwa miaka tisa [2009 hadi 2018], kabla ya kujizulu baada ya shinikizo kubwa kutoka ndani ya chama chake cha ANC.
Kama hao hawatoshi, yupo Robert Mugabe, ambaye akiwa mpinzani wa Serikali ya kikoloni nchini Zimbabwe aliwahi kuhukumiwa jela miaka 11.
Alikamatwa mwaka 1963 akituhumiwa kutoa kauli za uchochezi na alikuwa akihusishwa na harakati za uhuru. Alizuiliwa kwa takriban miaka 11 [1963 hadi 1974].
Zimbabwe ilipopata uhuru mwaka wa 1980, Mugabe akawa Waziri Mkuu. Mwaka 1987, akawa rasmi rais wa Zimbabwe, nafasi aliyoshika kwa miaka 30, kabla ya jeshi kumtoa madarakani mwaka 2017.
Vipi kuhusu Hastings Kamuzu Banda? Alikuwa kiongozi wa Nyasaland African Congress akiipinga Serikali ya kikoloni. Mwaka 1959, Banda akawa miongoni mwa viongozi wa Chama hicho waliokamatwa.
Alizuiliwa kwa takribani miezi 13, kuanzia Machi 1959 hadi Aprili 1960, kabla ya kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Malawi mwaka 1964 baada ya Taifa hilo kupata uhuru wake.
Malawi ilipokuwa jamhuri mwaka 1966, Banda alikuwa rais wa kwanza na kuhudumu kwa miaka 28 [1966 hadi 1994]. Aliondolewa madarakani baada ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1994.
Mbali na hao, historia haijamsahau Kwame Nkrumah aliyekuwa mmoja wa viongozi wakuu wa harakati za kupigania uhuru wa Ghana, wakati huo ikiitwa ‘Gold Coast’.
Mwaka 1950, alikamatwa na serikali ya kikoloni na kuhukumiwa kwa uchochezi na kufungwa jela lakini aliachiwa Februari 12, 1951, baada ya Chama chake, Convention People’s Party, kushinda uchaguzi wakati akiwa gerezani.
Alikaa gerezani kwa takribani mwaka mmoja, kisha akawa Waziri Mkuu wa Ghana baada ya Taifa hilo kupata uhuru mwaka wa 1957. Nchi hiyo ilipokuwa Jamhuri mwaka 1960, Nkrumah akawa rais wa kwanza.
Nkurumah alihudumu kama rais kwa muda wa maika sita [1960 hadi 1966] lakini alikuja kuondolewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi.
Hii ya kutoka jela hadi urais iliwahi kutokea pia kwa Jomo Kenyatta. Mwaka 1952, Serikali ya kikoloni ilifanya operesheni ya kuwakamata viongozi wa kisiasa wa Kenya, akiwamo Kenyata.
Kenyatta alihusishwa na uasi dhidi ya utawala wa kikoloni. Alikamatwa Oktoba 20, 1952, na kuzuiliwa hadi mwaka 1961.
Baada ya kuachiliwa huru, Kenyatta alitangazwa kuwa Waziri Mkuu wa Kenya mwaka 1963. Kenya ilipokuwa Jamhuri mwaka 1964, Kenyatta akawa rais wa kwanza wa taifa hilo, nafasi aliyohudumu kwa miaka 14 [1964 hadi 1978].
Nelson Mandela naye alikaa gerezani kwa miaka 27. Alijiunga na Chama cha African National Congress (ANC) na baadaye kuanzisha kikosi chake cha kijeshi, Umkhonto we Sizwe, ili kukabiliana na serikali ya kikoloni.
Mwaka wa 1962, Mandela alikamatwa na kuhukumiwa na kufungwa gerezani kwa miaka 27, hadi alipotolewa Februari 11, 1990. Alifungwa katika magereza kadhaa, likiwemo gereza la Robben Island.
Mei 10, 1994, aliapishwa kuwa rais wa Afrika Kusini na alihudumu kwa miaka mitano [1994 hadi 1999], kabla ya alistaafu kwa hiari baada ya kumaliza muhula mmoja.
Aidha, historia pia inatukumbusha kuhusu Abdoulaye Wade, ambaye kwa muda mrefu alikuwa mwanasiasa wa upinzani nchini Senegal.
Achilia mbali ile ya mwaka 1988, Wade alikamatwa tena mwaka 1994 baada ya kutuhumiwa kuhusishwa na mauaji ya afisa wa serikali.
Hata hivyo, kama ilivyotokea kwa wanasiasa wengine, mathalan Mandela, Wade alikuja kutoka gerezani na kuwa rais baada ya kushinda katika Uchaguzi wa mwaka 2000 na kuongoza kwa miaka 12 [2000 hadi 2012].
Makala haya ni kwa msaada wa Shirika la Utangazaji la Uingereza [BBC].


