Na Hassan Mwasha, Gazetini
MATAIFA tisa ya Afrika yameshajihakikishia tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia za mwakani zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico. Tunisia, Algeria, Ghana, Misri, Senegal, Afrika Kusini, Ivory Coast, Cape Verde na Morocco.
Makala haya yanawaangazia wawakilishi hao wa soka la Afrika kwa kuichambua Misri. Je, ina nafasi ya kufanya vizuri Kombe la Dunia?
Baada ya kuzikosa fainali zilizopita zilizofanyika mwaka 2022 nchini Qatar, Misri wamerejea Kombe la Dunia. Walifuzu baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Djibouti.
Misri iliongoza Kundi A ikiwa na pointi 26 baada ya mechi 10. Ni ushindi wa mechi nane na sare mbili. Waliifunga Guinea-Bissau bao 1-0 katika mchezo wa mwisho uliochezwa mjini Cairo.
Nahodha wa kikosi, Mohamed Salah, alikuwa na mchango mkubwa katika mechi za kufuzu, ambapo alizifumania nyavu mara tisa.
Amefikisha mabao 61 akiwa na timu ya Taifa, akibakiza nane tu kuwa mfungaji bora wa muda wote, rekodi ambayo kwa sasa inashikiliwa na kocha wake, Hossam Hassan.
Ukimuweka kando Salah, kikosi cha Misri kinajivunia ubora wa mastaa wengine, wakiwano Mahmoud Trezeguet, Zizo na Omar Marmoush, achilia uimara wa safu ya ulinzi iliyoruhusu mabao mawili pekee katika mechi 10.
Kocha wao, Hassan, aliyeajiriwa kuchukua nafasi ya kocha raia wa Ureno, Rui Vitoria, aliyefungashiwa virago baada ya Misri kuvurunda katika fainali za AFCON za mwaka 2024, naye ameandika historia ya aina yake.
Akiwa mchezaji, alifunga bao lililowapeleka Kombe la Dunia mwaka 1990. Hivyo, sasa anakuwa mtu pekee kuiwezesha Misri kufuzu michuano hiyo akiwa mchezaji na kocha.
Historia ya Kombe la Dunia inaitambua Misri kuwa ndiyo timu ya kwanza ya Afrika kushiriki Kombe la Dunia. Kumbukumbu zinaonesha kuwa ‘Mafarao’ walifanya hivyo mwaka 1934.
Hata hivyo, licha ya kushiriki mara nne kwenye mashindano hayo makubwa, Misri haijawahi kushinda mechi yoyote, achilia mbali kuvuka hatua ya makundi.
Hivyo basi, ndoto ya Salah na kocha wake, Hassan, ni kuona wanakuwa sehemu ya historia mpya ya Taifa lao kuvuka kwa mara ya kwanza hatua ya makundi na hata kufanya vizuri zaidi.
Published:


