Na mwandishi wetu, Gazetini
SERIKALI ya Afrika Kusini imekanusha kile kilichoelezwa na ripoti ya hivi karibuni ya Marekani, ikidai kuwapo kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hali ya ukiukwaji wa haki za binadamu imekuwa mbaya zaidi ndani ya mwaka huu, hasa baada ya Sheria mpya inayoipa Serikali nguvu ya kutaifisha mali za raia kwa matumizi ya umma.
Pia, ripoti ya Marekani ililaani migogoro ya ardhi inayoendelea nchini Afrika Kusini, ikitolea mfano tukio la wanawake wawili kuuawa wakiwa shambani, na kisha miili yao kuliwa na nguruwe.
Hata hivyo, wafuatiliaji wa siasa wanafahamu kuwa huu ni mwendelezo wa uhusiano mbaya kati ya uongozi wa Serikali ya Rais Donald Trump na Afrika Kusini.
Tayari Marekani imeshapandisha kwa asilimia 30 ushuru wa bidhaa za Afrika Kusini zinazozingia kwao. Hiyo imetajwa kuathiri uchumi wa Afrika Kusini kwa kiasi fulani.
Kabla ya ripoti hii, tayari Rais Trump aliinyoshea kidole Afrika Kusini akidai kuwa Serikali yake imekuwa ikisimamia ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya raia wachache wenye ngozi nyeupe (Afrikaners).
Hoja yake hiyo inaungwa mkono na bilionea wa Marekani, Elon Musk, aliyedai kuwa maelfu ya watu wenye ngozi nyeupe wameanza kuondoka katika Taifa hilo.
Kuthibisha madai hayo, Rais Trump alienda mbali zaidi kwa hatua yake ya kuanzisha programu maalumu ya kuwatafutia makazi nchini Marekani.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mchambuzi wa siasa wa Afrika Kusini, Hamilton Wende, anasema mtazamo huo juu ya Afrika Kusini ni sehemu ya siasa.
Madai ya Wende yanathibitishwa na takwimu, zikionesha kuwa ni wahamiaji wasiozidi 100 waliorudi Marekani kupitia programu hiyo ya Rais Trump.
Kwa upande wake, Idara ya Uhusiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini (DIRCO) imeeleza kushangazwa na hatua ya Marekani kuzungumzia masuala hayo wakati ilishajitoa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.
Wachambuzi wa siasa, akiwamo mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Rhodes cha Afrika Kusini, Thapelo Tselapedi, wanasema Marekani inajaribu ‘kuichafua’ Afrika Kusini kutokana na uhusiano wake mbaya na Israel.
Mwaka 2023, Afrika Kusini iliifungulia mashitaka Israel katika Mahakama ya Kimataifa (ICJ) ikiishutumu kwa mauaji yanayoendelea dhidi ya Wapalestina huko Gaza.
Tangu Afrika Kusini ilipoishitaki Israel, imekuwa ikiungwa mkono na mataifa kadhaa yasiyo na uhusiano mzuri na Marekani, ikiwamo Iran.
“Ni kwa maana hiyo, sasa Marekani inajaribu kuikomoa Afrika Kusini,” anasema Tselapedi na kukumbusha kuwa Israel ni mshirika mkubwa wa Marekani.
Published:


