Na mwandishi wetu, Gazetini
KATIKA siasa za Afrika na dunia kwa ujumla, Idi Amin ni mfano mzuri wa marais walioamua kuipuuza misingi ya demokrasia na utawala bora, na kisha kuzitawala nchi zao kwa ‘mkono wa chuma’.
Jumuhiya za kimataifa zinadai kuwa kati ya watu 100,000 na 500,000 nchini Uganda walipoteza maisha ndani ya miaka nane tu ya utawala wa Amin ulioanza mwaka 1971.
Katika makala haya, utapata kuvifahamu historia ya maisha ya kiongozi huyo; kabla, wakati na hata baada ya kuondoshwa madarakani mwaka 1979. Endelea …
Wengi wanamfahamu kwa jina la Idi Amin, lakini hicho ni kifupi tu. Jina lake kamili ni Awon’go Idi Amin Dada Oumee. Alizaliwa Mei 30, 1928.
Hata hivyo, kwa kuwa hakuandika kitabu na wala hakuruhusu waandishi kuchunguza maisha yake binafsi, kuna utata juu ya uhalisia wa siku yake ya kuzaliwa.
Kwa mujibu wa rekodi zilizoachwa na Serikali ya kikoloni ya Uingereza, ambayo kimsingi ndiyo iliyoitawala Uganda kabla ya uhuru, inasema Idi alizaliwa mwaka 1925.
Lakini, katika mahojiano yake ya mwaka 1972, Adi Amin alisema ana miaka 46, na hiyo ni sawa na mtu aliyezaliwa mwaka 1926. Hata hivyo, familia yake ina maelezo tofauti ikidai kuwa alizaliwa Mei 30, 1928.
Idi Amin alizaliwa katika Wilaya ya Nakasero Hill mjini Kampala. Baba yake alikuwa polisi na waliishi kwenye kota (nyumba za polisi).
Ifahamike kuwa jina la Idi Amin lilitokana na kuzaliwa Sikukuu ya Kiislam ya ‘Eid al-Adha’ inayosherehekewa baada ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Kwa mujibu wa mtafiti wa Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda, Fred Guweddeko, jina alilopewa na wazazi wake baada ya kuzaliwa ni Idi Awo-Ango Angoo.
Hakuwa mtoto pekee kwenye familia hiyo. Idi Amin alikuwa mtoto wa tatu wa kiume katika ndoa ya mzee Amin Dada Nyabira Tomuresu (1889–1976) wa Kabila la Kakwa, na bi. Aisha Chumaru Aate (1904-1970) aliyetokea Kabila la Lugbara.
Baba yake, Nyabira, alizaliwa katika familia ya Kikiristo ya Dhehebu la Katoliki, kabla ya kubadili Dini na kuwa Muislam mwaka 1910 na miaka mitatu baadaye alijiunga na jeshi la polisi la Uganda.
Kama ilivyokuwa kawaida ya wakoloni katika nchi zote walizotawala, Serikali ya Uingereza iliwakamata kwa nguvu vijana wa Uganda na kuwaingiza katika jeshi lake la King’s African Rifles.
Nyabira akawa miongoni mwao mwaka 1914 na kupelekwa kuisaida Uingereza katika Vita vya Kwanza vya Dunia mwaka 1914. Alipoachiwa mwaka 1921, ndipo alipojiunga na polisi. Alistaafu mwaka 1931.
Kwa upande wa mama yake Idi Amin, Aate, anatokea familia ambayo baba anatokea Kabila la Lugbara na mama ni wa Kabila la Kakwa.
Aate alikuwa mganga wa kienyeji na aliwahi kutibu tatizo la ugumba la aliyekuwa Malkia wa Buganda, Irene Drusilla Namaganda.
Historia inaleza kuwa Aate aliolewa na Nyabira (baba yake Idi Amin) akiwa mke wa pili baada ya yule wa kwanza kuwa na changamoto ya ugumba.
Hata hivyo, zipo taarifa zisizo rasmi kuwa baada ya Aate kumtibu Malkia Irene, ukaribu wake na familia ya Mfalme wa Buganda, Daudi Chwa II, ukawa mkubwa.
Hapo ndipo inaposadikika kuwa huenda Daudi Chwa II ‘alichepuka’ kwa siri na Aate, kisha ikatungwa mimba ya Idi. Kwamba Nyabira hakuwa baba mzazi wa Idi, bali alizungukwa bila kujua.
Usikose sehemu ya pili ya mfululizo wa simulizi hii … Tembelea www.gazetini.co.tz


