Na mwandishi wetu, Gazetini
HISTORIA inakumbusha, kwamba kwa amri ya Obote, Idi Amin aliongoza jeshi kuvamia makazi ya Kabaka, vurugu zilizosababisha vifo vya raia zaidi ya 1,000.
Katika kumfurahisha bosi wake, Idi Amin alipeleka sare za jeshi za Kabaka hadi ofisini kwa Obote. Kabaka alitoroka na kukimbilia Uingereza, ambako aliishi hadi alipofariki mwaka 1969.
Kama hiyo haitoshi, Idi Amin akiwa Mkuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, aliendeleza operesheni za kuhakikisha hakuna upinzani wala uanaharakati unaoupa changamoto uongozi wa Obote.
Hata hivyo, wakosoaji wa Idi Amin walidai kuwa alipendelea zaidi Wasudan Kusini, huku Waganda wakiwa wachache kwenye nafasi za utumishi wa jeshi.
Historia inaonesha kuwa Wasudan Kusini wamekuwa wakiishi kwa wingi Uganda tangu walipohamia wakati wa utumishi katika jeshi la kikoloni.
Kwa upande mwingine, ushawishi wa Idi Amin ndani ya jeshi na hata katika maeneo mengi ya Uganda, ukiwamo Mji aliozaliwa wa West Nile, vilianza kumpa wasiwasi Rais Obote.
Mwaka 1970, Obote alipiga hatua moja mbele kwa kutanga udhibiti wa vyombo vya dola. Hii ikawa ni pamoja na kupunguzia majukumu makubwa aliyokuwa nayo Idi Amin katika vyombo vya dola.
Wakati huo huo, Idi Amin alishashitukia kinachoendelea, ukiwamo mpango wa Obote kumkamata na kumfungulia mashitaka ya kutumia vibaya fedha za jeshi.
Januari 25, 1971, wakati Obote akiwa kwenye Mkutano wa Jumuhiya ya Madola uliofanyika Singapore, Idi Amin akaongoza jeshi kuipindua Serikali.
Kwa msaada wa Israel, wanajeshi wa Uganda wakaudhibiti Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe, kisha kushikilia Mji Mkuu wa Kampala. Wakazunguka makazi ya Obote, pamoja na kuzuia barabara zote kubwa.
Matangazo ya kuishutumu Serikali ya Obote kwa vitendo vya rushwa yakaanza kusikika katika vituo vya redio, kisha wananchi wakaingia barabarani kusherehekea anguko lake.
Idi Amin akaingia madarakani. Katika hotuba yake ya kwanza, alijiita mwanajeshi na si mwanasiasa, hivyo kuahidi kuwa jeshi lingeongoza kwa muda, kisha kupisha Uchaguzi ili wananchi waunde Serikali yao.
Kama hiyo haikutosha, ahadi nyingine ya Idi Amin ikawa ni kuwaachia wafungwa wote wa kisiasa waliotupwa magerezani wakati wa utawala wa Rais Obote.
Je, Idi Amin ataziishi ahadi zake? Wapi alikosea? Bado kuna mengi ya kuyafahamu juu ya maisha yake, hasa miaka yake nane ya kuiongoza Uganda.
Usikose sehemu ya nne ya mfululizo wa simulizi hii … Tembelea www.gazetini.co.tz


