PRETORIA, Afrika Kusini
TEMBO wanatajwa kuwa ndiyo wanyama walio hatarini zaidi katika vitendo vya ujangili duniani kote, huku Afrika ikichomoza katika takwimu hizo.
Kwa mujibu wa takwimu, miaka 100 iliyopita imeshuhudia asilimia 90 ya tembo barani Afrika wakiuawa kwa lengo la kujipatia meno, pembe na ngozi.
Mwaka 2016, tani zaidi ya 100 ya pembe za tembo zilikamatwa na kuchomwa moto mjini Nairobi, Kenya, idadi kubwa zaidi kuwahi kutokea.
Kama hiyo haitoshi, ripoti ya programu ya Ufuatiliaji wa Mauaji ya Tembo (MIKE) ya mwaka 2017 ilibaini kuwa asilimia 40 waliuawa kwa ujangili.
Aidha, Ripoti ya Taasisi ya IFAW inaeleza kuwa pembe za tembo zimekuwa zikihitajika kwa kiwango cha juu, hasa katika mataifa yaliyoendela barani Asia.
Ni kama ilivyobanishwa na utafiti uliofanywa na Taasisi ya C4ADS mwaka 2023, uliozitaja nchi za Asia kuhusika kwa kiasi kikubwa katika ununuaji wa siri wa meno na pembe za tembo.
“Lengo kubwa la ujangili wa tembo ni kupata pembe, ambazo hutumika kutengeneza mapambo, vito na dawa za asili,” inaeleza ripoti hiyo.
C4ADS wanawataja tembo aina ya ‘Loxodonta cyclotis’ wanaopatikana Botswana, Cameroon, Gabon, DRC, Guinea ya Ikweta, Ivory Coast, Liberia na Ghana, kuwa ndiyo walio hatarini zaidi.
Inaelezwa kuwa aina hiyo ya tembo imepungua kwa asilimia 86 katika kipindi kifupi tu cha miaka 31iliyopita.
Kwa upande mwingine, ripoti inafafanua ukubwa tatizo hilo kwa kuitaja Botswana kuwa ni moja ya mataifa hatari zaidi katika ujangili wa tembo barani Afrika.
Katika ripoti hiyo, IFAW inaeleza kuwa vitendo vya ujangili wa tembo vimekuwa vikifanyika hata kwenye hifadhi za taifa. “Hii inatia shaka kuona mamlaka za Serikali zinashindwa kudhibiti vitendo hivi,” inaeleza ripoti hiyo.
Hata hivyo, bado tatizo hilo limeonekana kwa kiwango cha kutisha katika mataifa ya Ethiopia (18.4%), Nigeria (17.6%), DRC (8.8%) na Msumbiji (8.8%).
Lakini, Msumbiji, kama ilivyo kwa Angola, zimeathiriwa zaidi na kiwango kikubwa cha ujangili uliopo kwa majirani zao, Namibia na Afrika Kusini.
Katika utafiti wa mwaka 2017, kushindwa kumudu gharama za maisha kulitajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa vitendo hivi vya ujangili.
Kati ya watu 173 walihojiwa na kukiri kujihusisha na ujangili, 164 walisema wangeachana na vitendo hivyo endapo wangekuwa na njia zingine za kuingiza kipato cha kuendesha maisha yao.
Kwa kulifahamu hilo, IFAW imekuwa ikizalisha fursa za kujikwamua kuchumi katika maeneo yaliyo na matukio mengi ya ujangili.
Mathalan, Taasisi hiyo ina mradi wa ‘Jenga Mama’ nchini Kenya, ambao unatoa mafunzo ya ufundi kwa wanawake wa kabila la wamasai ili kuwainua kiuchumi.
Wakati huo huo, IFAW wana mradi wa Chikolongo nchini Malawi, ambao umewezesha upatikanaji wa maji-safi, ufugaji wa samaki na kilimo cha kisasa.
“Pia, tuna mradi wa Zambia unaoendesha programu za mafunzo ya kilimo cha kisasa ili kuinua maisha ya wakulima,” inaeleza taarifa ya IFAW.


