23.1 C
New York

NIC yajivunia dhamana ya bilioni 292, RC Mtanda aipa mtihani

Published:

Na Mwandishi wetu, Mwanza

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Justine Mwandu amesema kwa sasa shirika lina mtaji mkubwa wa Sh bilioni 15 na mali na dhamana mbalimbali zinazofikia Sh bilioni 292 ambazo zimelifanya kuwa imara kiuchumi na kuwa tayari kukinga bima za miradi mikubwa ya maendeleo.

Mwandu amesema hayo Mei 27, 2025 jijini Mwanza wakati wa ziara ya wajumbe wa bodi hiyo na menejimenti ya shirika hilo walipotembelea baadhi ya wateja wao wakubwa ikiwemo Bodi ya Pamba (TCB), Shule ya Msingi Nyakahoja, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico) kwa ajili ya kuwashukuru na kuimarisha mahusiano.

Amesema tayari shirika hilo limesimamia bima za miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo daraja la Kigongo-Busisi, Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, Reli ya Kisasa (SGR), huku likiwa tayari kutoa huduma hiyo kwenye mradi wa ujenzi wa meli kubwa ya MV Mwanza inayotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.

“NIC ina mtaji wa kutosha Serikali ilikubali kutuongezea mtaji kupitia faida zetu na ina assets (mali) na uwekezaji wa kutosha, tunawekeza kwenye dhamana mbalimbali za mabenki, Serikali zikiwemo bondi na hizo assets zingine zinaifanya NIC iwe imara zaidi kiuchumi,” amesema Mwandu

Akizungumzia lengo la ziara hiyo, Mwandu amesema ni kukutana na wateja na wadau wakubwa wa kibiashara wa shirika hilo ambao wamekuwa wakiwaunga mkono, kuzungumza nao na kufahamu changamoto zinazowakabili ili kuzitatua na kuendeleza ushirikiano baina yao.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda (kushoto) akizungumza na wajumbe wa bodi ya wakurugenzi na menejimenti ya Shirika la Bima la Taifa (NIC) walipomtembelea ofisini kwake jijini Mwanza ili kutoa shukrani za kuwa mteja wa shirika hilo, kuzungumza na kusikiliza changamoto zinazowakabili. Picha na Mwandishi wetu

“Tumekuja kuwahakikishia commitment yetu tuendelee kufanya kazi pamoja kuna miaka kadhaa tuliteteleka lakini sasa tuko vizuri tuna mtaji mzuri na hata mali zetu ziko vizuri tumekuja kutoa shukrani na kuwaomba kuendelea kushirikiana ili kuwapa huduma stahiki,” amesema Mwenyekiti huyo

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico), Erick Khamis amelihakikishia shirika hilo kuwa wako tayari kushirikiana katika kufanya ukaguzi na kupata gharama za bima inayopaswa kulipwa kwa ajili ya Meli ya MV Mwanza kwani bima ni moja ya masharti yanayopaswa kutekelezwa ili meli hiyo iliruhusiwe kuanza safari.

“Wamekuja wakati muafaka ambapo tunahitaji bima kama moja ya masharti ya kukamilisha meli iweze kubeba abiria, kwahiyo wataangalia watafanya hesabu waangalie aina ya gharama tutakazolipa ili tupate hiyo bima iliyokusudiwa kwa hii meli na kuifanya sasa itembee tukiwa tumepata vibali vyote,” amesema Hamis

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amelitaka shirika hilo kuacha kutegemea miradi ya Serikali ambayo wana uhakika wa kuipata na badala yake wachangamkie fursa za miradi mipya na sekta binafsi ili kushindana na mashirika mengi ya kibinafsi.

“Msilale mko sokoni mna ushindani na wenzenu miradi ya Serikali mnaweza kuwa na uhakika wa kuipata lakini miradi binafsi lazima muichangamkie, kwa kuwa ni taasisi ya Serikali tumieni utaalam wenu na uhakika wa mtaji mkubwa mlionao kushawishi wadau, hapa Mwanza kwa sasa kuna miradi mikubwa inaendelea na kuna uwekezaji katika sekta ya usafiri ndani ya Ziwa Viktoria kwahiyo muwekeze nguvu hapa,” amesema Mtanda

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Marko Mutunga ameipongeza Serikali kwa kuliimarisha shirika hilo, huku akiahidi kulifanyia kazi suala la kukata bima ya maisha kwa wafanyakazi wa bodi hiyo.

“Ni jambo la kushukuru kwamba chombo cha Serikali kinafanya vizuri kwenye ushindani kuna vitu vingine vilivyoongezeka hususan kwenye sekta ya kilimo vinavyohitaji bima. Tumelichukua hili la bima ya maisha kwa wafanyakazi tutaona jinsi ya kulifanyia kazi, pia bado kuna eneo la kushughulikia na kupanua biashara zaidi kati ya Bodi ya Pamba na Shirika la Bima,” amesema Mutunga

Mmoja wa wateja wa shirika hilo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyakahoja jijini Mwanza, Sista Judith Damian amelipongeza kwa namna ambavyo linashughulikia kwa wakati malipo ya madai ya wateja wake wanapopata changamoto mbalimbali zikiwemo za ajali.

“Tumekuwa na ushirikiano mzuri na NIC tunajua umuhimu wa bima kwa sababu ajali ama janga linakujia muda wowote, kwa mfano mwaka 2021 magari yetu yalipata ajali lakini bima ilifanya kazi yake na yakatengenezwa kwa wakati. Bima imekuwa muhimu kwetu na tunaahidi kuendeleza ushirikiano huu,” amesema Sista Judith.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img