Na Mwandishi Wetu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea na mikakati ya kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na wa Mataifa mbalimbali duniani ikiwamo Japan ili kuwawezesha kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo katika mataifa hayo.
Majaliwa amesema kuwa Serikali imekuwa ikifanya hivyo kwa kushiriki katika makongamano mbalimbali ya kimataifa ambayo yamekuwa yakiwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji ili kuongeza tija kubwa kwenye masuala ya biashara na uwekezaji.

Amesema hayo leo Mei 26, 2025, alipofungua kongamano la Biashara, Uwekezaji na Utalii lililowakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na wafanyabiashara na wawekezaji wa Japan katika Osaka, Japan ikiwa ni sehemu ya ushiriki wa Tanzania katika maonersho ya World Expo Osaka 2025.
“Tumewaeleza wafanyabaishara na wawekezaji hawa wa Japan fursa ambazo zipo nchini, hii ni mara ya tatu tunakutana na wafanyabara na wawekezaji kutoka Japan, tayari tumeanza kuona manufaa ya makongamano haya kutokana na kuongezeka kwa biashara kati ya mataifa haya mawili,” amesema.

Amesema hadi Machi 2025, jumla ya kampuni 24 kutoka Japan zimewekeza nchini katika miradi mbalimbali yenye thamani ya Dola 42.70 milioni za Marekani (sawa na Sh 115 bilioni) nchini na kutoa ajira 1,182 kwa Watanzania.
Majaliwa amesema licha ya uwekezaji wa makampuni hayo, Serikali ya Tanzania imeendelea kunufaika na ushirikiano wake na Japan kwa kupata misaada katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo na miundombinu.


