22.6 C
New York

Simchimba aitaka Ligi Kuu, tatu zamfuata

Published:

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

MSHAMBULIAJI wa Geita Gold, Andrew Simchimba amemaliza mkataba wake na timu hiyo na sasa amefungua milango ya kurejea Ligi Kuu Bara, huku timu tatu tayari zikiwa zimeshamfuata kuanza mazungumzo ya kumrejesha kwenye ligi hiyo.

Simchimba ambaye ameng’ara kwenye Ligi ya Championship msimu wa mwaka 2024/2025 akimaliza kinara wa mabao akifunga 18 sawa na Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar na Abdulaziz Shahame wa TMA, akiiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi ya nne.

Simchimba aliyewahi kutamba na Ihefu na KMC kwenye Ligi Kuu Bara alikiri imkataba wake wa mwaka mmoja na Geita Gold aliousaini mwanzoni mwa msimu huu umemalizika na sasa yuko tayari kwa ukurasa mpya baada ya kuichezea timu hiyo mechi 21 za ligi.

Nyota huyo anasubiri mchezo wa mtoano (play-off) kusaka nafasi ya kupanda Ligi Kuu, ambapo Geita Gold itamenyana na Stand United, mchezo wa kwanza ukipigwa Uwanja wa Nyankumbu Mei 24, mwaka huu na marudiano kuchezwa Kambarage, Shinyanga Mei 28, 2025.

“Mkataba wangu na Geita Gold umemalizika nipo huru na nia yangu ni kucheza Ligi Kuu Bara kwa sababu nilikuja huku Championship kurejea kiwango change baada ya kukumbwa na majeraha,” alisema Simchimba.

Aliongeza kuwa; “Zipo timu zinakuja zinataka mazungumzo na mpaka sasa tayari timu tatu zimenifuata na zote ni za Ligi Kuu bila shaka mambo yakikamilika tutajulishana kinachoendelea.”

Simchimba anaungana na mshambuliaji mwenzake kikosini hapo, Yusuph Mhilu aliyemaliza wa pili kwa kupachika mabao kikosini hapo (10) ambaye pia mkataba wake wa mwaka mmoja unamalizika mwishoni mwa msimu huu.

Geita Gold ilimaliza katika nafasi ya nne kwenye Ligi ya Championship ikivuna alama 56 katika mechi 30, ikishinda 17, sare tano na kupoteza nane huku ikifunga mabao 51 na kuruhusu 26.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img