10.6 C
New York

Magenge ya uhalifu yanavyoitesa Serikali ya Mexico – [5]

Published:

SINALOA, Mexico

MAGENGE hayo ya uhalifu wa dawa za kulevya nchini Mexico hayajiendeshi kienyeji, na badala yake yana mifumo yake ya kuyasaidia kuvuna ushawishi katika jamii na kujiimarisha dhidi ya nguvu ya vyombo vya dola.

Kugawa vyakula kwa raia na kuendesha akaunti za mitandao ya kijamii, ikiwamo WhatsApp na Telegram, ni miongoni mwa zana wanazotumia kujiendesha kisasa kama zilivyo taasisi zingine.

Ndani ya magenge hayo, vipo vitengo maalumu vyenye wataalamu wa kuratibu operesheni na kutengeneza propaganda za kuyasafisha dhidi ya shutuma.

Pia, magenge hayo yamekuwa yakishinikiza vyombo vya Habari kwa kuwatisha, kuwateka na kuwaua waandishi wanaoripoti mabaya yao.

Wakati huo huo, yanajivunia baadhi ya viongozi wa serikali ‘wanaokula nao’ kwa siri, kama ilivyowahi kutokea skendo ya Katibu wa Usalama wa Taifa, Genaro Garcia Luna, ambaye alibainika kupokea rushwa kutoka kwao na kufunguliwa mashitaka nchini Marekani.

‘Pax Mafioso’ ni skendo nyingine kubwa ya ukaribu uliopo kati ya viongozi wa serikali na magenge hayo. Ni skendo ya wanasiasa kuyatumia magenge hayo kuvuna ushawishi wa kura kipindi cha uchaguzi.

Kwamba baada ya magenge hayo kumsimamia mwanasiasa fulani na hatimaye akashinda, basi hatoyagusa maeneo yao yenye mtandao wa biashara ya dawa za kulevya na uhalifu mwingine.

Mwaka 2005, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (PGR) ilieleza kuwa takribani watumishi 1,500 wa Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai walikuwa wakijihusisha na vitendo vya uhalifu chini ya magenge hayo.

Miaka ya hivi karibuni imeshuhudia serikali ya Mexico ikiendesha operesheni na hata kuwafungulia mashitaka baadhi ya maofisa wa polisi katika maeneo mbalimbali, ikiwamo Nuevo Laredo, Michoacán, Baja California na Mexico City.

Mwaka 2006, Rais Calderon alianzisha operesheni ya kusaka silaha za polisi katika maeneo yote jeshi hilo lilipohusishwa kufanya kazi na magenge ya halifu.

Miezi michache baadaye, alifumua jeshi la polisi katika majimbo yote 31, ambapo aliwaondosha kazini makamanda 284.

Kilichofuata katika operesheni hiyo ni kutiwa nguvuni kwa maofisa wengi wa polisi waliotajwa kuvujisha taarifa za kiusalama kwa magenge hayo kwa lengo ya kuyalinda dhidi ya mkono wa sheria.

Miongoni mwa majina makubwa yaliyotikisa wakati wa kamatakamata hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Jeshi la Kimataifa [Interpol] nchini Mexico, Ricardo Gutierrez Vargas.

Pia, lilikuwepo jina la Julio Cesar Godoy Toscano, ambaye alishinda kiti cha ubunge mwaka 2009. Alikamatwa baada ya kuvuja kwa taarifa kuwa ni mmoja ya viongozi wa juu wa La Familia Michoacana, moja ya magenge hatari ya uhalifu.

Ni kama ripoti moja ilivyowahi kueleza mwaka 2010, kwamba Sinaloa Cartel walikuwa wakitumia vyombo vya dola kudhohofisha wapinzani wake wa biashara ya dawa za kulevya.

Licha ya kuwapo kwa madai ya uhusiano wao na magenge hayo, viongozi wa serikali ya Mexico wamekuwa wakikausha kila ilipotokea wakaulizwa kuhusu hilo.

Itaendelea …

Related articles

Recent articles