Na Editha William Gazetini – KAGERA
KATIBU wa UVCCM Kata ya Hamgembe, Sharifu Idirisa, amemshukuru Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Bakoba, Eston James, kwa mchango wake wa kuwezesha upatikanaji wa Uwanja wa Bunena utakaotumika kwa mchezo wa fainali ya mashindano ya soka ya Muhaj Cup 2026.
Akizungumza kuhusu hatua ya mashindano hayo, Sharifu ambaye pia ni Katibu wa Mashindano hayo, amesema fainali ya Muhaj Cup 2026 inatarajiwa kuchezwa kesho, Novemba 29, 2026, kwenye Uwanja huo ulioko Kata ya Bakoba.
Katika mchezo wa fainali, Omukishenye FC itaivaa Mchikichini FC baada ya timu hizo kuzifunga Kashabo FC na Fenicha FC kwenye mechi mbili za hatua ya nusu fainali.
Kabla ya mechi hio, linatarajiwa kuchezwa bonanza la madereva wa bodaboda kutoka maeneo ya Kashabo na Omukishenye na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu kati ya Fenicha na Kashabo FC.
Kwa upande wake, Sharifu amesema viongozi mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo ya kimichezo itakayokuwa sehemu ya kuhitimisha mashindano hayo ya Muhaj Cup kwa mwaka huu wa 2026.


