SINALOA, Mexico
GENGE jingine la uhalifu wa dawa za kulevya lenye historia kubwa nchini Mexico ni Beltran-Leyva Cartel. Kundi lililonzishwa na ndugu wanne; Marcos Arturo, Carlos, Alfredo na Hector.
Mwaka 2004 na 2005, Arturo aliliongoza kundi hilo katika mapigano ya mara kwa mara dhidi ya Sinaloa Cartel. Walikuwa wakigombea udhibiti wa mtandao wa unga katika eneo la Kaskazini-Mashariki mwa Mexico.
Zipo taarifa za uhakika zinazodai kuwa genge hilo lilikuwa na mizizi kwenye serikali, mahakama na hata polisi na hiyo ililipa uhuru wa kuendesha operesheni zake za uhalifu.
Mwaka 2009, kiongozi wake, Arturo, aliuawa na huo ukawa mwanzo wa uhasimu wa ndugu watatu waliobaki, kila mmoja akitaka kuongoza.
Tofauti na wakati ule wa Arturo, kundi lilianza kupoteza nguvu yake mbele ya wapinzani [magenge mengine ya uhalifu], ikiwamo washirika wake kujiengua na kuanzisha falme zao.
Hatimaye, kundi hilo lilipotea moja kwa moja baada ya kiungo wake wa mwisho, Hector Beltran Leyva, kukamatwa na polisi Oktoba, 2014.
Achilia mbali Beltran-Leyva Cartel, Juarez Cartel ni kundi jingine la kihalifu lenye historia kubwa na ya aina yake katika biashara ya dawa za kulevya nchini Mexico.
Kundi hilo lilivuma zaidi kuanzia mwaka 2007, likiongozwa na Ciudad Juarez, huku yakiwepo madai ya kupewa nguvu na baadhi ya maofisa waandamizi wa vyombo vya dola, hasa polisi.
Mwaka 2014, kundi hilo lilipata pigo baada ya aliyekuwa kiongozi wake wakati huo, Vicente Carrillo Fuentes, kukamatwa na tangu hapo halijaweza kuwa na nguvu kubwa.
Makundi mengine ni Tijuana Cartel, Gulf Cartel, Los Zetas, La Familia Michoacana Cartel, Knights Templar Cartel, na Jalisco New Generation Cartel.
Itaendelea …


