12.1 C
New York

Serikali yawa mwanahisa mkubwa TMRC kwa Sh bilioni 17.76

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini – DAR

SERIKALI imekuwa mwanahisa mkubwa zaidi wa Kampuni ya Mikopo ya Nyumba Tanzania (TMRC), baada ya kununua asilimia 27.73 ya hisa za kampuni hiyo, zenye thamani ya Sh bilioni 17.76, katika hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa mikopo ya nyumba ya muda mrefu na yenye gharama nafuu nchini.

Kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), Serikali imepata hisa 12,166,674 na kuwa kinara miongoni mwa wanahisa 21 wa kampuni hiyo, yenye mtaji uliolipwa wa Sh bilioni 56.02.

Hati ya umiliki wa hisa hizo imekabidhiwa Novemba 27, 2026, jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TMRC, Theobald Sabi, kwa Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu.

Akizungumza kabla ya kupokea hati hiyo, Mchechu alisema Serikali imeamua kuwa mwanahisa wa kimkakati ili kuiwezesha TMRC kupata fedha za muda mrefu na zenye gharama nafuu, kuongeza imani ya wawekezaji na kuchochea upatikanaji wa makazi bora, ambayo ni miongoni mwa vipaumbele vya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

“Makazi ni chachu ya amani na ukuaji wa uchumi wa nchi. Tuna wajibu wa kuwainua Watanzania wengi ili kudumisha amani,” amesema Mchechu, akisisitiza kuwa uwekezaji huo ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa nyumba nchini.

Alisema imani ya wawekezaji kwa Tanzania inatokana na sera nzuri za kiuchumi, huku akiitaka TMRC kutumia mazingira hayo kujipambanua zaidi kwa kuendelea kutoa hati fungani ili kupata mitaji ya kufadhili mikopo ya nyumba.

Aidha, aliitaka kampuni hiyo kushirikiana na benki kubuni bidhaa mpya za kifedha zitakazowawezesha wananchi wengi zaidi kumudu gharama za kupata nyumba.

Kwa upande wake, Sabi amesema ununuzi wa hisa hizo unaonesha imani ya Serikali kwa TMRC na kuongeza uwezo wa kampuni hiyo kusaidia benki na taasisi nyingine za fedha kutoa mikopo ya nyumba ya muda mrefu kwa gharama nafuu.

“Huu si uwekezaji kwenye nyumba pekee, bali katika mapambano dhidi ya umaskini, kwani sekta ya nyumba inabeba sekta nyingine nyingi,” alisema Sabi, akiahidi kuwa Bodi itaendelea kusimamia taasisi hiyo kwa weledi.

Mikopo ya nyumba yafikia Sh bilini 209.47

Mkurugenzi Mtendaji wa TMRC, Elibariki Ndossi, alisema hadi Septemba 30, 2026, kampuni hiyo ilikuwa imezikopesha benki na taasisi za fedha Sh bilioni 209.47, sawa na takribani asilimia 26 ya soko la mikopo ya nyumba nchini.

Alisema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 128.2 bilioni zilitokana na Mradi wa Kufadhili Mikopo ya Nyumba (HFP) uliotekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.

Mradi huo ulianza mwaka 2010 kwa mkopo wa masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 40 kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa (IDA), kabla ya kuongeza ufadhili hadi takribani dola milioni 100 na kufungwa Juni 28, 2019.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), iliyokuwa taasisi tekelezi ya mradi huo, iliipa TMRC leseni mwaka 2011 na inaendelea kuisimamia chini ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 pamoja na Kanuni za Makampuni ya Kufadhili Mikopo ya Nyumba za mwaka 2022.

Ndossi alisema tangu kuanzishwa kwake, mtaji wa TMRC umeongezeka kutoka Sh2.9 bilioni hadi Sh56.02 bilioni, huku idadi ya benki zinazotoa mikopo ya nyumba ikiongezeka kutoka tatu hadi 30.

Hata hivyo, alionya kuwa ukuaji wa mikopo ya nyumba hauendani na kasi ya upatikanaji wa nyumba zinazokidhi mahitaji ya wananchi.

“Fedha za mikopo peke yake hazijengi nyumba. Nyumba lazima zijengwe kwanza, kwa bei ambayo wananchi wanaweza kumudu, ndipo mikopo ya nyumba iwe na maana,” alisema.

Tanzania yakabiliwa na upungufu wa nyumba milioni nne

Takwimu alizowasilisha zinaonesha ukubwa wa changamoto ya makazi nchini. Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi ya Watu (UN-Habitat) linakadiria kuwa Tanzania ina upungufu wa takribani nyumba milioni nne, huku Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikikadiria mahitaji ya nyumba mpya kuwa 391,000 kila mwaka.

Kwa mujibu wa takwimu za wizara hiyo, mwaka 2022 Tanzania ilikuwa na takribani nyumba milioni 14.7 kwa watu milioni 61.7.

Hata hivyo, mahitaji yanatarajiwa kuongezeka kutokana na ukuaji wa idadi ya watu. Ifikapo mwaka 2050, idadi ya Watanzania inatarajiwa kufikia milioni 118.1, huku mahitaji ya nyumba yakikadiriwa kufikia milioni 26.8.

Wakati huohuo, sehemu ya watu wanaoishi mijini inatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 34.9 mwaka 2022 hadi asilimia 59 ifikapo mwaka 2050, hali inayoongeza shinikizo la mahitaji ya makazi katika maeneo ya mijini.

Changamoto hiyo inaonekana pia katika mazingira ya makazi yaliyopo. Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 inaonesha kuwa asilimia 43.1 ya kaya za mijini zina chumba kimoja tu cha kulala, huku ni asilimia 12.2 pekee ya kaya hizo zikiwa na hati miliki.

Katika soko la fedha, mikopo ya nyumba bado ina nafasi ndogo ikilinganishwa na ukubwa wa uchumi. Deni la mikopo hiyo ni asilimia 0.45 tu ya Pato la Taifa, huku wastani wa mkopo mmoja ukifikia Sh138 milioni.

Ingawa viwango vya riba vimeshuka kutoka asilimia 20 hadi 24 na kufikia asilimia 13 hadi 18, bado gharama hizo ni changamoto kwa kaya nyingi zinazotaka kumiliki nyumba.

Changamoto ya makazi ni ya dunia nzima

Ndossi alisema changamoto ya upatikanaji wa makazi bora haipo Tanzania pekee, bali ni suala linaloikabili dunia.

Kwa mujibu wa UN-Habitat, takribani watu bilioni 2.8 duniani hawana makazi bora ya kutosha, huku zaidi ya bilioni 1.1 wakiishi katika makazi duni.

Barani Afrika, asilimia 62 ya makazi ya mijini si rasmi, huku Benki ya Shelter Afrique ikikadiria kuwa bara hilo lina upungufu wa nyumba zaidi ya milioni 53.

Ili kukidhi mahitaji ya makazi duniani ifikapo mwaka 2030, inakadiriwa kuwa nyumba takribani 96,000 zinapaswa kujengwa kila siku.

Akizungumzia hatua za kukabiliana na changamoto hiyo nchini, Ndossi alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi, ikiwamo kupitia Sera ya Taifa ya Ardhi, kuondoa kodi katika ujenzi wa nyumba zenye thamani ya chini ya Sh50 milioni na kuboresha utoaji wa hati za umiliki wa sehemu ya jengo (unit titles).

Ofisi ya Msajili wa Hazina na TMRC zimesema zitaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha, BoT na taasisi za fedha kujenga mfumo imara na endelevu wa ufadhili wa makazi.

Naye Naibu Gavana wa BoT anayesimamia Uthabiti wa Sekta ya Fedha, Sauda Msemo, aliyemwakilisha Gavana wa benki hiyo, alisema wanatarajia TMRC kuendeleza mchango wake katika kuboresha sekta ya makazi na mfumo wa fedha nchini.

“TMRC ni wakala muhimu katika kutekeleza Dira 2050 kwani ni mdau mkubwa katika ukuaji wa sekta ya makazi,” amesema.

Related articles

Recent articles