Na Malima Lubasha, Gazetini – SERENGETI
WAZAZI wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mapinduzi, wilayani Serengeti, mkoani Mara, wamewataka walimu kuendelea kuwalea wanafunzi katika misingi ya maadili mema ya Kitanzania, wakieleza kuwa malezi bora yanachangia nidhamu, bidii katika masomo na mafanikio ya kitaaluma.
Wito huo umetolewa katika mkutano wa wazazi uliofanyika viwanja vya shule hiyo mjini Serengeti, kujadili maendeleo ya taaluma, kupokea taarifa ya matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba wa mwaka 2026 na kuweka mikakati ya kuboresha ufaulu kwa mwaka 2027.
Wazazi hao wamewapongeza walimu kwa matokeo mazuri yaliyopatikana katika mitihani ya ngazi ya kata, wilaya, mkoa, Kanda ya Ziwa na Taifa, wakisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya walimu na wazazi katika kusimamia maendeleo ya wanafunzi.
Wamesema mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni, kufanya mazoezi ya kutosha, kufanya mitihani ya mara kwa mara, kudhibiti utoro na kuongeza muda wa ufundishaji imechangia kuboresha matokeo.
Wazazi Samson Melengo, Juma Ntagira na Mabula Lucas wamesema wataendelea kushirikiana na walimu kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora, huku wakiahidi kufuatilia mahudhurio ya watoto wao na kazi za ziada wanazopewa wanapokuwa nyumbani.
“Tunatoa pongezi kwa uongozi wa shule na walimu kwa kazi nzuri ya matokeo ya mtihani wa Darasa la Saba 2026, ambapo wanafunzi wote wamefaulu kwa madaraja A hadi C. Muendelee kutoa chakula shuleni na kusimamia taaluma ipasavyo. Walimu wanapotimiza wajibu wao na kutokea changamoto, msisite kutoa taarifa kwa wazazi na ngazi nyingine za Serikali,” wamesisitiza.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Jumanne Nyamhanga, amesema mafanikio yaliyopatikana yametokana na mikakati iliyowekwa kwa pamoja na wazazi na walimu, ambao wametekeleza wajibu wao katika ufundishaji, utoaji wa mazoezi na kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni.
Amesema chakula kimechangia kuboresha usikivu wa wanafunzi darasani, huku akiwataka wazazi kutembelea shule mara kwa mara ili kutoa ushauri kuhusu maendeleo ya taaluma, kusaidia kudhibiti utoro na kushirikiana na uongozi wa shule kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Nyamhanga, ambaye anaongoza shule yenye wanafunzi 1,322 na mikondo zaidi ya 20, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mikutano ya wazazi, hususan kwa walezi wa wanafunzi wa Darasa la Nne na la Saba wanaotarajiwa kufanya mitihani.
Naye Mwalimu wa Taaluma na Maadili wa shule hiyo, Samwel Meso, amesema taarifa ya maendeleo ya taaluma kwa mwaka 2026 inaonesha kuwa shule ilipata wastani wa daraja B katika mtihani wa majaribio wa ngazi ya wilaya, daraja A katika mtihani wa mkoa na daraja B katika ngazi za kata na Kanda ya Ziwa.
Akizungumzia matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba mwaka 2026, Meso amesema wanafunzi wote 124 waliofanya mtihani huo wamefaulu kwa asilimia 100, wakipata madaraja kuanzia A hadi C, huku shule ikipata wastani wa alama 200.69.


