Na mwandishi wetum Gazetini-DAR
SERIKALI ya Tanzania imesisitiza kutounga mkono mapendekezo yanayotaka kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja na kuondoa adhabu kwa makosa ya kujamiiana kinyume na maumbile, ikieleza kuwa msimamo huo unazingatia sheria za nchi, mila, desturi, tamaduni na maadili ya jamii ya Kitanzania.
Waziri wa Katiba na Sheria, Abdallah Ulega, leo Jumapili, Novemba 15, 2026 kuwa Serikali itaendelea kusimamia sheria zilizopo na kuzingatia maadili ya jamii katika kufanya maamuzi yanayohusu masuala ya haki za binadamu.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha msimamo wa Tanzania kuhusu mapendekezo yaliyotolewa katika mchakato wa Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu kwa Nchi (UPR), chini ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Ulega amesema:
“Serikali ya Tanzania haitounga mkono mapendekezo yanayokwenda kinyume na sheria za nchi, mila, desturi, tamaduni na maadili ya jamii ya Kitanzania.”
Katika mchakato huo, Tanzania imeeleza kutounga mkono jumla ya mapendekezo 68 yaliyotolewa na nchi mbalimbali, kwa sababu zinazohusisha tofauti za misimamo ya kitaifa na hitaji la kufanya tathmini zaidi.
Ulega amesema baadhi ya mapendekezo hayo yanahitaji utafiti na mashauriano ya kina ili kubaini athari zake za kisheria, kisera, kijamii na kiuchumi kabla ya kufikiwa kwa maamuzi.
Ameongeza kuwa maamuzi kuhusu kuridhia mikataba ya kimataifa na kufanya mabadiliko ya sheria yanayogusa maisha ya wananchi yanapaswa kufuata taratibu za kikatiba na kuhusisha mamlaka husika.
“Masuala yanayohusu mabadiliko ya sheria na kuridhia mikataba ya kimataifa yanapaswa kufuata taratibu za kikatiba na kuhusisha mamlaka zinazohusika, ikiwemo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.


