5.4 C
New York

Koffi Olomide: Msomi wa uchumi, mama alimpa jina la mume wa mtu – [1]

Published:

KINSHASA, DRC

ANAITWA Antoine Christophe Agbepa Mumba, lakini tasnia ya burudani inamfahamu zaidi kwa jina la Koffi Olomide, mkongwe wa muziki wa Rhumba na muasisi wa bendi maarufu ya Quartier Latin International.

Mbali na sauti nzuri ya kuimba, pia Koffi raia wa DRC ni mtunzi, dansa na prodyuza mwenye jina kubwa ndani ya nchi hiyo, Afrika na ulimwengu kwa ujumla, wengine wakimwita ‘Mopao’, ‘Mfalme wa Ndombolo’ na majina mengi ya utani.

Anatajwa kuwa mmoja ya wanamuziki wakubwa kuwahi kutokea barani Afrika katika karne ya 20, ngoma zake zikigusa mapenzi, siasa, teknolojia, mafanikio na wakati mwingine imani za dini.

Anapotajwa kama miongoni mwa wasanii wakubwa, inamaanisha Koffi ana nyimbo zaidi ya 300, pia akiwa na tuzo sita za Kora, zikiwamo nne alizobeba kwa mpigo mwaka 2002, pamoja na ile ya Lejendari wa AFRIMA [2021].

Historia yake iko hivi; Koffi alizaliwa Julai 13, 1956, huko Stanleyville, Mji ulioko Kaskazini-Mashariki mwa DRC, na sasa ukifahamika kwa jina la Kisangani. Baba yake, Charles Agbepa, ni raia wa nchi hiyo, wakati mama yake, Aminata Angelique Muyonge, ni wa Sierra Leone.

Baada ya Koffi kuzaliwa, baba aliiacha familia kwa muda mrefu, hali iliyosababisha maisha yawe magumu kwa mama yake, ambaye sasa alilazimika kusaidiwa na majirani ili kumudu chakula.

Pia, kutokana na mdororo wa afya ya mama yake, Koffi akiwa bado mchanga alianza kunyonyeshwa na jirani yao. Ni kutokana na kuthamini mchango huo, ndipo mama yake akamitwa Antoine, jina la mume wa jirani huyo.

Kwa wasiofahamu, ‘Koffi’ ni Ijumaa kwa lugha ya Akan, siku ambayo mwanamuziki huyo alizaliwa. Vilevile, ‘Olomide’ ni jina la utani la mjomba wake, hivyo Koffi alilichukua tu na kuanza kulitumia kwenye muziki.

Tukirudi kwenye maisha ya utoto, baadaye baba yake, Charles, ambaye alikuwa mfanyabiashara, alirejea na kuishi na familia yake katika mitaa ya Lemba, Kinshasa, hadi walipohamia Lingwala mwaka 1973.

Wakiwa huko, Koffi alianza kufuzuia ndoto zake za maisha lakini haikuwa muziki. Alitamani kucheza soka la kulipwa, kama baba yake alivyowahi pia kuitumikia AS Vita ya Ligi Kuu ya DRC.

Hata hivyo, Koffi alianza kuufuatilia muziki baada ya kusikiliza na kukoshwa na nyimbo za mastaa wa Enzi hizo, wakiwamo Zaiko Langa Langa, Franco Luambo, Le Grand Kalle, Vicky Longomba, na Tabu Ley Rochereau.

Kwa baba yake, haikuwa rahisi kumruhusu Koffi kujihusisha na muziki, na badala yake alitamani asome tu. “Baba yangu aliniambia kama nataka kuwa mwanamuziki, basi lazima kwanza niwe na Shahada [Degree ya Chuo Kikuu].

Mwaka 1974, akiwa na umri wa miaka 18, Koffi alifaulu vizuri na kwenda kusoma masomo ya biashara katika Chuo Kikuu cha Bordeaux kilichoko Kusini-Magharibi mwa Ufaransa.

Lakini, wakati huo tayari alishaingiwa na damu ya muziki, hivyo akiwa chuoni aliweza kutengeneza gitaa na kujifunza namna ya kulicharaza, pia kuandika nyimbo kadhaa.

Aliporejea DRC wakati wa likizo ya masomo ya chuo, Koffi hakulala, akaanza kuwaandikia nyimbo baadhi ya wasanii wa Kinshasa na kujipatia jina la ‘mwanafunzi maarufu zaidi nchini Zaire [DRC].

Akiwa bado likizo, hatimaye Koffi aliachia ngoma yake ya kwanza iitwayo ‘Sango Ndambo’ na ‘Asso’. Wakati huo, alishakutana na Papa Wemba, ambaye naye bado alikuwa anajitafuta akiwa mwandishi wa nyimbo, kama alivyokuwa Koffi.

Sasa, wawili hao wakajikuta wakiwa karibu na hata baada ya Papa Wemba kuanzisha bendi maarufu ya Viva La Musica mwaka 1977, Koffi alihusika kuandika ngoma kadhaa, zikiwamo ‘Mere Superieure’ na ‘Ebalé Mbonge’.

Februari, 1978, Koffi aliachia ngoma nyingine kali, ‘Princesse ya Synza’, akisaidiwa na Viva La Musica ya Papa Wemba. Kuanzia hapo, zikafuata ‘Samba Samba’, ‘Ekoti ya Nzube’, ‘Elengi ya Mbonda’, ‘Bien Aimee’ na ‘Anibo’.

Hatimaye, Koffi alihitimu masomo ya Chuo Kikuu na kutunukiwa Shahada ya Uchumi wa Biashara mwaka 1981, hivyo kurudi Kinshasa kwa ajili ya kuanza kutafuta ajira.

Itaendelea …

Related articles

Recent articles