LONDON, Uingereza
BONDIA chipukizi raia wa Uingereza, George Francis, ameeleza kusikitishwa na kitendo cha kuikosa michuano ya dunia ya U-19 ya mwaka huu baada ya kutokuwepo kwa uthibitisho juu ya jinsia yake.
Francis mwenye umri wa miaka 18, ambaye anapigana uzito wa Kilogramu 60, alitarajiwa kushiriki mashindano hayo yaliyofanyika Oktoba, 2026, mjini Budva, Montenegro.
Hata hivyo, mzaliwa huyo wa Loughton, Essex, alishindwa kushiriki baada ya waratibu kukosa uthibitisho juu ya jinsia yake.
“Waliniita chumbani na kuniambia kwamba nisingeweza kushiriki kwa sababu hawakuwa wakifahamu kama mimi ni mwanaume au mwanamke,” amesema Francis akihojiwa na kituo cha televisheni cha BBC Sport.
Aidha, ‘dogo’ huyo amewatupia lawama viongozi wa timu yake akisema walizembea kupeleka vipimo vya uthibitisho wa jinsia kwa waratibu wa mashindano hayo.
“Nilielezwa kwamba [viongozi wangu] hawakupeleka vipimo vya damu kwa wakati. Wenzangu wote walifanyiwa hivyo, ni mimi tu niliyekosekana,” amesema.
Bondia huyo chipukizi amesema ilimuuma kukosa mashindano hayo kwani alishajiandaa vya kutosha kuhakikisha anafanya vizuri na kutwaa ubingwa.
“Ilikuwa ni habari mbaya kuwahi kuisikia kwenye maisha yangu,” amesema na kuongeza: “Kwa kweli, nisingependa hii imtokee mtu mwingine.”


