Na mwandishi wetu, Gazetini-Shinyanga
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba amepiga marufuku kuchangishwa kwa fedha za mafuta ya magari ya dharura yanayobeba wagonjwa, akielekeza ambulansi zote katika hospitali kuhakikisha zinakuwa na mafuta wakati wote ili wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka wasikwame kupata rufaa kwa kukosa fedha za mafuta.
Akizungumza leo Jumatatu, Novemba 9, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Solwa, mkoani Shinyanga wakati wa ziara yake ya kikazi ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi, Dk. Mwigulu amesema Serikali imewekeza katika huduma za afya, lakini baadhi ya watumishi wanadhoofisha juhudi hizo kwa kuendeleza uzembe na mazoea.
Amesema ambulansi zilizonunuliwa na Serikali zinapaswa kuwa tayari wakati wote kuwahudumia wagonjwa, badala ya ndugu wa mgonjwa kuombwa kuchanga fedha za mafuta kabla ya safari ya kwenda hospitali ya rufaa.
“Ambulensi ipo na ina dereva na analipwa na Serikali na ni mwajiriwa wa Serikali lakini mgonjwa amesha andikiwa na daktari kwamba anatakiwa apelekwe hospitali ya rufaa tena haraka lakini wandugu wanaambiwa nendeni mkakae kule mchangishane fedha ya mafuta..tusichangishe fedha ya mafuta kwenye ambulensi imbebe mgonjwa imuharakishe hospitalini,” amesema.
Amesema mgonjwa aliye mahututi na kuandikiwa rufaa ya haraka hapaswi kuambiwa asubiri ndugu zake wachangishane fedha za mafuta, akisisitiza kuwa magari hayo siyo daladala zinazochangishwa fedha ya mafuta badala yake zinapaswa kuwa tayari wakati wote kwa ajili ya kuokoa maisha.
“Ambulansi zote ziwe na mafuta, bajeti iwekwe…na sasa hivi mnaandaa bajeti nataka ambulansi zote ziwe standby. Mgonjwa ambaye anatakiwa kunusuliwa maisha yake asiombwe fedha ya mafuta. Tunamuombaje mtu mahututi fedha ya mafuta na anatakiwa akimbizwe kwa dharura?,” amehoji.
Ameonya kuwa watumishi watakaobainika kuomba fedha za mafuta kwa wagonjwa mahututi watachukuliwa hatua, akieleza kuwa serikali haiwezi kuvumilia uzembe unaoweza kuhatarisha maisha ya wananchi.
Aidha, ameagiza wajawazito wanaofika hospitalini wakiwa na uchungu wasicheleweshwe kwa sababu ya taratibu za kutafuta vifaa kama beseni au ndoo, bali wahudumiwe haraka na kufikishwa kwa daktari.
Katika mkutano huo pia amezungumzia upatikanaji wa dawa hospitalini, akitaka vyombo vya ulinzi na usalama kusaidia kufuatilia fedha zinazotolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, dawa zinazonunuliwa na namna zinavyowafikia wananchi.
Amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya dawa, lakini bado baadhi ya wagonjwa wanaelekezwa kwenda kununua dawa katika maduka ya nje ya hospitali, hali inayoongeza mzigo kwa familia ambazo hazina uwezo wa kumudu gharama za vipimo na matibabu.

Ameagiza kufuatiliwa kwa fedha hizo kuanzia zinapotolewa hadi dawa zinaponunuliwa na kusambazwa, ili kubaini sababu zinazowafanya wananchi kuendelea kukosa dawa katika vituo vya kutolea huduma.
Kilio cha Pamba, Mifugo
Katika hotuba yake, Dk. Nchemba ametangaza kuwa kuanzia msimu ujao wa mavuno ya pamba, Serikali haitaruhusu mfumo wa mnunuzi mmoja katika maeneo husika, akisema wanunuzi wengi wataruhusiwa ili kuongeza ushindani na kuinua bei kwa manufaa ya wakulima.
Amesema alilipokea suala hilo wakati wa ziara yake mkoani Simiyu, ambako alielezwa kuwa mfumo wa mnunuzi mmoja ulikuwa ukichangia kushuka kwa bei ya zao hilo na kumuelekeza Waziri wa Kilimo kukutana na wadau na kutafuta utaratibu utakaowanufaisha wakulima.
Amesema lengo ni kuhakikisha pamba inarejesha hadhi yake kama dhahabu ya Kanda ya Ziwa na wakulima wanapata bei inayostahili kwa mazao yao.
Kuhusu mifugo, Waziri Mkuu amesema Serikali imefuta sheria iliyokuwa ikitumika kusimamia utaifishaji wa mifugo, hatua aliyosema inalenga kuwalinda wafugaji dhidi ya kupoteza mifugo yao.
Ameongeza kuwa amezielekeza Wizara ya Fedha na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha wafugaji ambao mifugo yao ilichukuliwa na kuuzwa kwa mnada, lakini baadaye wakashinda kesi mahakamani, wanarejeshewa fedha zao.
Amesema kiasi cha zaidi ya sh bilioni 3.8 kinapaswa kurejeshwa kwa wafugaji hao na Wizara ya Fedha imeanza kutekeleza maelekezo hayo.
Dk. Mwigulu amesema Serikali imechukua hatua ya kufuta kodi kwenye baadhi ya malighafi zinazotumika kutengeneza saruji, akisema hatua hiyo inalenga kupunguza gharama za uzalishaji na hatimaye bei ya saruji kwa wananchi.
Asikiliza changamoto za wananchi
Katika mkutano wake na wananchi wa Solwa, Dk. Mwigulu Nchemba amepokea malalamiko mbalimbali kuhusu madai ya malipo ya kazi, migogoro ya ardhi, uchimbaji madini na huduma za kijamii, huku akitoa maelekezo kwa viongozi na watendaji wa Serikali kuyafanyia kazi.
Akiwasilisha changamoto yake, Bakari Rwanda amelalamikia kutolipwa fedha za kazi za ufundi alizofanya katika shule za Mwasingo na Mwambasha, akidai zaidi ya sh milioni 1.1.
Akijibu malalamiko hayo, Dk. Mwigulu ameelekeza mwananchi huyo alipwe stahiki zake, huku kasoro zilizobainishwa katika kazi alizofanya zikifanyiwa marekebisho.
Mwananchi mwingine, John Ruhende mkazi wa Mwang’osha mkoani humo amewasilisha malalamiko kuhusu tofauti za taarifa za eneo la shamba lake zilizokuwa kwenye nyaraka ambapo Dk. Mwigulu amemuelekeza Mwanasheria kufuatilia suala hilo na kuchunguza tofauti zilizopo katika nyaraka ili hatua stahiki zichukuliwe.
Akielezea mgogoro wa uchimbaji madini katika kitaru namba sita Mwakitoliyo, Shija Nangale amesema licha ya kuchimba mgodi namba sita tangu mwaka 1994 na baadaye Serikali kuunda vikundi vya wachimbaji mwaka 2024 hawajasajiliwa licha ya maeneo mengine kuanzia namba moja hadi namba tano kupewa kusajiliwa.
“Namba sita tulipotaka kusajili mwenyekiti wa kijiji akakataa kuwa hii ni hifadhi ya kijiji tukae kwanza halmashauri ya kijiji tutawaambia,”amesema.
Amesema matokeo yake wakashangaa amepewa leseni mwekezaji mwingine, miliki wa leseni hiyo, Rahma Abdallah ameeleza kuwa alikuwa tayari kushirikiana na wachimbaji hao, lakini kulikuwa na kutokuelewana.
Dk. Mwigulu amesema atamtuma Waziri wa Madini, Anthony Mavunde kufuatilia suala hilo na kuwakutanisha wahusika ili kutafuta suluhu ya mgogoro huo.


