Na mwandishi wetu, Gazetini – SHINYANGA
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amemwelekeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga kuharakishaujenzi wa jengo la huduma za dharura (Emergency) katika Hospitali ya Wilaya hiyo.
Dk Nchemba ametoa maelekezo hayo leo Jumanne Novemba 10, 2026, baada ya kupokea hoja ya Mbunge wa Kahama Mjini, Benjamini Ngayiwa, kuhusu umuhimu wa Hospitali hiyo kuwa na jengo maalumu la dharura.
Akitoa maagizo ya utekelezaji wa hoja hiyo, Dk. Mwigulu amemtaka Mkurugenzi kuanza taratibu za kitaalamu na manunuzi kabla ya mwisho wa Mwaka wa Fedha 2026-2027.
Amesema maandalizi ya mradi huo yanapaswa kufanyika mapema ili ujenzi wake uanze kwa wakati uliopangwa, hatua inayolenga kuboresha huduma za matibabu kwa wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa haraka.
“… Nakuepekeza Mkurugenzi kabla ya kumalizika kwa Mwaka huu wa Fedha, taratibu zote za kitaalamu, pamoja na taratibu za manunuzi, zikamilishwe ili tunapoanza mwaka ujao tuwe tayari kwa ujenzi wa jengo hilo na wananchi wa Kahama na maeneo jirani wanufaike na huduma bora za dharura,” amesema Dk. Mwigulu.
Awali, akitoa salamu za jimbo mbele ya waziri Mkuu, Ngayiwa aliiomba Serikali kuipandisha hadhi Hospitali ya Manispaa ya Kahama kuwa ya Mkoa, sambamba na ujenzi wa jengo la dharura ili kukidhi utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ngayiwa alisema Manispaa ya Kahama ina muingiliano mkubwa wa watu, ikiwemo magari yanayokwenda katika nchi za Burundi, Rwanda, Uganda na DRC, hali inayosababisha msongamano mkubwa wa huduma za afya.
“Tunakuomba sana tupate jengo la wagonjwa wa dharura lenye ubora. Ukizingatia Kahama kuna muingiliano mkubwa wa watu, magari yanayoenda Burundi, Rwanda, Uganda, Congo yote yanapita hapa,” alisema Ngayiwa.


