13.6 C
New York

Yanga kumenoga, hizi hapa mashine mbili alizotua nazo Fadlu

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

BAADA ya kutua rasmi Yanga, kocha wa zamani wa Simba, Fadlu Davids, ameongozana na ‘Wasauzi’ wengine wawili, huku mwingine akitarajiwa kumfuata kwa ajili ya kumsaidia majukumu yake pale Jangwani.

Fadlu aliyetoka Raja Casablanca, amejiunga na Timu ya Wananchi kuchukua mikoba ya kocha mwenzake raia wa Afrika Kusini, Manqoba Mngqithi, ambaye alifungashiwa virago hivi karibuni.

‘Mashine’ mbili alizotua nazo Fadlu asubuhi ya leo Novemba 7, 2026, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere ni Darian Wilken na Mueez Kajee.

Mbali na hao, kocha msaidizi mwingine anayetarajiwa kumfuata hivi karibuni ni Maahier Davids, huku Simo Dladla aliyekuwa na Mngqithi akitarajiwa kuendelea na kazi Jangwani.

Kama itakumbukwa, Wilken, Kajee na Maahier waliwahi kufanya kazi na Fadlu katika klabu zote mbili zilizopita, kwa maana ya Simba na Raja Casablanca.

Mashabiki wa soka la Tanzania hawajasahau kuwa Fadlu aliiongoza Simba kutwaa kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, pamoja na kuisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

YANGA WALIVYOMNASA

Katika hatua nyingine, Fadlu alifichua kuwa Yanga walifanya majaribio mawili ya kuinasa saini yake, kabla ya kufanikiwa safari hii. Wanajangwani wameinasa huduma yake akiwa anawaniwa na MAS Fes ya Morocco.

“Nimefurahi, naiona Tanzania kama nyumbani. Watu wa Tanzania wamekuwa wakinipokea na kunionesha upendo mkubwa. Ni jambo zuri sana kurudi na kujiunga na klabu hii kubwa,” amesema Fadlu.

Pia, kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 ameweka wazi mikakati yake ya kuendeleza mafanikio makubwa ya Yanga katika soka la ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

“Tunataka kutengeneza aina ya uchezaji, falsafa ya uchezaji, kuboresha hatua kwa hatua, kuendeleza mafanikio na kuifanya Yanga kubaki juu,” amesema kocha huyo wa zamani wa Orlando Pirates.

VITA NA BARKER

Fadlu anatua Yanga na kuwakuta wapinzani wao, Simba, wakiwa kwenye mwendelezo wa kiwango bora chini ya kocha mwenzake raia wa Afrika Kusini, Steve Barker.

Kwa sasa, Simba wako kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa tofauti ya pointi tano, huku kila timu ikiwa imeshashuka dimbani mara 10.

Hata hivyo, licha ya kikosi cha Yanga kuandamwa na majeraha, Fadlu anaamini bado wana nafasi ya kushindana na kurejea kileleni. “Hatutopoa hadi pale tutakaporudi kileleni,” amesema.

ACHIMBA MKWARA LIGI YA MABINGWA

Taarifa zinaeleza kuwa Yanga itaweka kambi ya muda mfupi Visiwani Zanzibar, ambako Fadlu na benchi lake la ufundi watapata muda wa kuangalia maboresho yanayohitajika kikosini.

Wakati huo huo, Fadlu anaikuta Yanga ikiwa imeshatinga hatua ya makundi, ambako imeangukia kundi lenye Zamalek [Misri], MC Alger [Algeria] na Club Africain [Tunisia].

“Tuna michuano ya Ligi ya Mabingwa mbele yetu lakini kama nilivyosema, mimi ni kocha mwenye matarajio makubwa. Naitazama Ligi ya Mabingwa, ingawa kila mmoja anasema tuko kwenye ‘kundi la kifo. Hakuna kinachoshindikana,” amesema.

Related articles

Recent articles