18.2 C
New York

Nyama ya digidigi yampeleka jela miaka 20

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

ATHUMANI Issa Rashid, mkazi wa Same mkoani Kilimanjaro mwenye umri wa miaka 47, amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kupatikana na nyara za Serikali, zikiwemo nyama za wanyamapori wawili aina ya digidigi.

Mbali na hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Same juzi Novemba 3, 2026, pikipiki moja aliyokuwa akitumia Athuman nayo imetaifishwa na Serikali.

Hukumu hiyo imekuja baada ya Mahakama kujiridhisha na ushahidi uliowasilishwa katika kesi ya uhujumu uchumi namba ECO 16343/2026 iliyofunguliwa dhidi ya mshtakiwa huyo.

Mshitakiwa alikamatwa Julai 12, 2026 katika eneo la Msitu wa Mabilioni, wilayani Same, na askari wa uhifadhi wa TANAPA waliokuwa katika doria ya kudhibiti ujangili na makosa mengine ya jinai.

Wakati huo, Athuman alikuwa na nyama za wanyamapori wawili aina ya digidigi wanaotajwa kuwa na thamani ya Dola za Marekani 600 [Shilingi 1,574,100 za Tanzania].

Baada ya kukamilika kwa uchunguzi, mshtakiwa alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Same Julai 17, 2026, na kusomewa shitaka la kupatikana na nyara za Serikali.

Related articles

Recent articles