18.2 C
New York

Wazazi washauriwa lishe bora, mtindo wa maisha watajwa

Published:

Na Editha William, Gazetini

WAZAZI na walezi wamekumbushwa kuzingatia lishe bora, hasa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wakihimizwa kuzingatia makundi sita ya vyakula.

Aidha, mtindo wa maisha, ikiwamo ‘ubize’ wa kazi, umetajwa kuwa na athari kubwa katika upatikanaji wa lishe bora.

Hayo yamezungumzwa na Afisa lishe, Idara ya Afya, Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera, Gisela Richard, akisema makundi sita hayo ya vyakula ndiyo yanayokamilisha mlo kamili.

“Kundi la kwanza ni nafaka, mizizi yenye wanga na ndizi mbichi. Kundi la pili ni asili ya wanyama na mazao yake, pamoja na wadudu wanaoliwa. Kundi la tatu ni jamii ya mikunde, karanga na mbegu zenye mafuta.

“Kundi la nne ni matunda, mfano machungwa, maembe, matikiti maji n.k. Kundi jingine ni mbogamboga na kundi la mwisho ni mafuta,” amesema Gisela.

Aidha, ameongeza kuwa athari za kukosa lishe bora ni pamoja na magonjwa ya uzito uliokithiri, shinikizo la damu [pressure], kisukari, figo kufeli, na saratani.

Katika hatua nyingine, Gisela ameishauri jamii kuzingatia vyakula vya asili, hasa vinavyotoka mashambani kwani vina vitamini na madini ya kutosha, ikilinganishwa na vilivyosindikwa.

“Hivi vya viwandani mara nyingi vinakuwa vimeongezewa kemikali na wakati mwingine vinakuwa vimekaa muda mrefu, hivyo kwenye matumizi ya binadamu vinaweza visiwe rafiki na kupelekea kupata magonjwa,” amesema.

Related articles

Recent articles