21.8 C
New York

Mkuyu Africa yalenga nyumba 3,000, Mwigulu atoa wito

Published:

MOSCOW, URUSI

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, amewataka vijana na wafanyabiashara Watanzania kutumia maarifa, teknolojia na fursa wanazozipata katika majukwaa ya kimataifa kuchochea uwekezaji, ubunifu na maendeleo ya kiuchumi nchini.

Wito huo aliutoa wakati wa Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika na Urusi (Russia–Africa Summit), uliofanyika Moscow, nchini Urusi, ambako alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Katika ziara hiyo, Dk. Mwigulu alikutana na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Tanzania walioshiriki katika mkutano wa kibiashara kati ya Tanzania na Urusi uliofanyika pembezoni mwa mkutano huo, kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo.

Mkutano huo uliangazia fursa za ushirikiano katika sekta mbalimbali, zikiwemo nishati, kilimo, madini, ujenzi na miundombinu.

Akizungumza na wafanyabiashara hao, Waziri Mkuu aliwahimiza kutumia maarifa waliyoyapata, teknolojia waliyojifunza na mahusiano waliyojenga na wadau wa kimataifa kuanzisha na kukuza shughuli za kiuchumi nchini.

Alisisitiza pia umuhimu wa vijana kujenga uwezo wa kujitegemea kiuchumi na kushiriki katika uzalishaji mali, badala ya kutegemea ajira pekee.

MKUYU AFRICA YAPANGA MIRADI YA MAKAZI 3,000

Miongoni mwa washiriki wa mkutano huo alikuwa Mwanzilishi na Afisa Mtendaji Mkuu wa MKUYU Africa, Juneid Othman, ambaye amesema kampuni hiyo ina mpango wa kutekeleza miradi ya zaidi ya nyumba 3,000 za kisasa katika maeneo ya mijini, kwa ajili ya kuuza na kupangisha.

Juneid alisema mpango huo unalenga kuchangia upatikanaji wa makazi bora, kukuza uwekezaji katika sekta ya majengo na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya miji nchini.

Alieleza kuwa MKUYU Africa inakusudia kutekeleza miradi hiyo kwa kushirikiana na wabia mbalimbali wa ndani na nje ya nchi katika sekta ya nyumba na ujenzi.

Kwa mujibu wake, matumizi ya teknolojia za kisasa, ubunifu katika usanifu wa majengo na ushirikiano na wawekezaji wenye uzoefu ni miongoni mwa mambo yatakayosaidia kufanikisha mipango hiyo.

Alisema dira ya kampuni ni kuchangia maendeleo ya miji yenye makazi na majengo ya biashara yanayokidhi mahitaji ya sasa na yajayo, huku yakizingatia viwango vya kisasa vya ujenzi na miundombinu.

KUIMARISHA ELIMU YA UWEKEZAJI NA SEKTA YA MAJENGO

Mbali na shughuli za ujenzi kupitia MKUYU Africa, Juneid anashiriki katika kutoa elimu kuhusu uwekezaji na usimamizi wa mali isiyohamishika kupitia jukwaa la MILIKI MALI, linalolenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu mali, fedha na fursa za uwekezaji.

Pia, kupitia Tanzania Brokers Association Board (TBAB), amekuwa akihusishwa na jitihada za kuimarisha taaluma ya udalali kwa kuhimiza uwazi na weledi katika sekta ya mali isiyohamishika.

Juneid alisema maendeleo ya sekta ya majengo yanahitaji ushirikiano wa wadau, elimu sahihi ya uwekezaji, mifumo inayowezesha biashara na matumizi ya teknolojia ili kuongeza ufanisi na kuimarisha imani ya wawekezaji.

FURSA ZA KIMATAIFA KUFUNGUA MILANGO YA UWEKEZAJI

Juneid aliishukuru Serikali kwa kuwezesha vijana na wafanyabiashara kushiriki katika mikutano ya kimataifa kupitia uratibu wa Tanzania Private Sector Foundation (TPSF), akisema majukwaa hayo yanatoa nafasi ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga mahusiano ya kibiashara na wawekezaji wa mataifa mbalimbali.

Alisema ushiriki wao umewawezesha kupata maarifa kuhusu matumizi ya teknolojia katika kukuza biashara na kujenga mitandao ya wabia wanaoweza kuchangia upatikanaji wa mitaji na fursa mpya za uwekezaji nchini.

Aliongeza kuwa mahusiano hayo yanaweza kusaidia kuchochea shughuli za kiuchumi, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wananchi kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali.

Kwa upande wa MKUYU Africa, mipango ya miradi ya makazi na majengo ya biashara inaweka msisitizo katika kutumia ushirikiano, teknolojia na ubunifu kupanua shughuli zake katika sekta ya ujenzi Afrika Mashariki.

Ushiriki wa wafanyabiashara vijana katika majukwaa ya kimataifa unatoa fursa ya kuunganisha maarifa, mitaji na teknolojia na mahitaji ya ndani. Hata hivyo, matokeo ya fursa hizo yatategemea namna zitakavyogeuzwa kuwa uwekezaji na miradi inayotekelezeka na yenye manufaa kwa uchumi wa Tanzania.

Related articles

Recent articles