Na mwandishi wetu, Gazetini
MWANAHARAKATI wa Tanzania na mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Twaha Mwaipaya, anadaiwa kutekwa na watu wenye silaha katika eneo la Kamulu, nje kidogo ya Jiji la Nairobi, nchini Kenya, huku wasiwasi ukiongezeka kuhusu usalama wake na mahali alipo.
Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, Mwaipaya aliripotiwa kutekwa leo Jumapili, Oktoba 25, 2026, saa nne asubuhi akiwa safarini kwa teksi kwenda kuwatembelea marafiki zake katika eneo hilo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa watu wanaodaiwa kumteka walikuwa wakitumia magari matatu, likiwemo gari aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop.
“Twaha Mwaipaya, raia wa Tanzania, aliripotiwa kutekwa na watu waliokuwa wakisafiri kwa magari matatu, ikiwemo Toyota Land Cruiser Hardtop, wakati akisafiri kwa teksi kuwatembelea marafiki,” imesema taarifa ya Amnesty International.
Taarifa za kupotea kwa Mwaipaya zimeibua wasiwasi miongoni mwa wanaharakati wa haki za binadamu, akiwemo Maria Sarungi, ambaye amesema anashirikiana na taasisi zinazohusika na haki za binadamu katika juhudi za kumtafuta.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari, Mawasiliano na Uenezi wa Chadema Taifa, Brenda Rupia, amezitaka mamlaka husika nchini Kenya kuchukua hatua za haraka kubaini mahali alipo Mwaipaya na kuhakikisha usalama wake.
“Tunaziomba mamlaka husika kwa haraka kubaini alipo, kuhakikisha usalama wake wa mara moja, na kuwachukulia hatua wahusika. Yeyote mwenye taarifa anahimizwa kujitokeza mara moja kutoa taarifa. Usalama wa Twaha lazima uwe kipaumbele, familia yake na umma wanastahili majibu,” amesema Rupia kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Hadi sasa, bado hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na mamlaka za usalama nchini Kenya kuhusu madai ya kutekwa kwa Mwaipaya.


