4.9 C
New York

Tshisekedi amshambulia Kabila kwa kujiunga na waasi

Published:

KISHANSA, Congo

RAIS wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Félix Tshisekedi, amemkosoa vikali mtangulizi wake, Joseph Kabila, baada ya kuongoza rasmi vuguvugu la kisiasa na kijeshi la Front pour la refondation de la nation (FRN), linalohusisha makundi ya waasi yanayopambana na Serikali ya Kinshasa.

Tshisekedi ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano na wabunge na maseneta wa muungano wake wa kisiasa wa Union sacrée mjini Kinshasa, Jumamosi, Oktoba 24, 2026, akijibu mabadiliko ya hivi karibuni katika uongozi wa vuguvugu hilo.

Akizungumza mbele ya viongozi hao, Tshisekedi alimshutumu Kabila kwa kuchagua kutumia silaha dhidi ya nchi aliyokuwa akiiongoza kwa miaka 18. Alimtaja kuwa “mwoga”, akisema hatua yake ya kujiunga na uasi inaonesha kuwa hakuwahi kuwa na mapenzi ya dhati kwa taifa hilo.

Hata hivyo, Tshisekedi aliwahakikishia wabunge na maseneta wa muungano wake kuwa hali ya usalama nchini humo iko chini ya udhibiti, huku akieleza kuwa Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) linaendelea kuimarika na kupambana na waasi licha ya changamoto zinazoendelea katika maeneo ya mapigano.

Wito wa kubana matumizi

Katika mkutano huo, Tshisekedi pia amewataka viongozi na wananchi kubana matumizi ili kusaidia kugharamia operesheni za kijeshi mashariki mwa nchi na kutekeleza miradi ya maendeleo ya Serikali yake.

Kuhusu mazungumzo ya kitaifa yanayotarajiwa kufanyika, aliwataka wabunge na maseneta kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wake, akisisitiza kuwa lengo ni kurejesha hali ya kawaida nchini na kuweka msingi wa amani ya kudumu.

Akizungumzia Katiba, Tshisekedi amesema dhamira yake ni kurejesha nchi katika hali nzuri na kuhakikisha amani inadumu. Alieleza kuwa hataki kutumia mchakato wa mazungumzo kama njia ya kujiongezea muda wa kukaa madarakani, huku akisema suala la mabadiliko ya Katiba ni jukumu la viongozi na taasisi husika.

Kabila alitangaza rasmi kuongoza FRN Oktoba 12, 2026, mjini Goma, mashariki mwa DRC. Vuguvugu hilo lilitokana na muungano wa AFC/M23 na linajumuisha viongozi wa kisiasa na kijeshi wanaopinga Serikali ya Tshisekedi. Hatua hiyo imeongeza mvutano wa kisiasa na kiusalama nchini humo wakati juhudi za kidiplomasia za kumaliza mapigano mashariki mwa nchi zikiendelea.

Related articles

Recent articles