Na Hassan Mwasha, Gazetini
HUENDA si uamuzi uliowashangaza wengi Yanga kumfuta kazi kocha wake raia wa Afrika Kusini, Manqoba Mngqithi. Uamuzi huo umekuja muda mfupi tu baada ya suluhu [0-0] dhidi ya TRA United.
Hatua hiyo imekuja baada ya tetesi za muda mrefu, kwamba Manqoba asingemaliza msimu huu wa 2026-27 akiwa kwenye benchi la ufundi. Zipo sababu zilizomponza kocha huyo. Ni zipi?
Mosi, kupoteza ‘Kariakoo Derby’. Kutoka suluhu na TRA United kunaweza kusiwe tatizo. Shida ni kwamba hii ni mechi ya pili mfululizo kwenye bila ushindi. Kabla ya kukutana na TRA United, Yanga ilifungwa mabao 2-1 na Simba.
Kwa timu inayohitaji kutetea ubingwa wake wa Ligi, si afya sana kudondosha pointi tano katika mechi mbili. Hii imewafanya mabosi wa Yanga waamke usingizini ‘fasta’ na kufanya maamuzi.
Pili, kiwango kibovu cha timu. Kama ni takwimu za ushindi, basi Manqoba hakustahili kufukuzwa. Ameshinda mechi 10 kati ya 13 alizokaa kwenye benchi, akitoa sare mbili na kufungwa moja tu.
Shida ni namna timu inavyocheza. Hata pale Yanga ilipopata ushindi, mashabiki hawakuwahi kuondoka uwanjani wakiwa na furaha. Hawakuwa wakiiona timu yao ‘ikitembea’ uwanjani kama walivyozoea chini ya makocha wengi waliopita.
Tatu, ubutu wa safu ya ushambuliaji. Licha ya Yanga ya Manqoba kutokucheza soka la kuvutia, bado iliweza kutengeneza nafasi nyingi za mabao ndani ya uwanja. Utumiaji wa nafasi ukawa tatizo, ambalo pia lilionekana vizuri hata katika mechi yao dhidi ya TRA United.
Nne, presha ya nje. Hata kama uongozi wa Yanga ulitamani kumvumilia, joto la mashabiki lilishapanda kwa kiasi kikubwa, hasa kuelekea mechi yao dhidi ya TRA United.
Mara zote, viongozi hutaka kubaki salama kwenye nafasi zao, hivyo namna pekee ya kufanikiwa katika mazingira ya aina hii ni ‘kumtoa kafara’ yule anayenyooshewa kidole na mashabiki.
Katika hilo la presha ya nje, ubora wa Simba kwa sasa unaweza kuhusishwa pia. Kiwango na matokeo yao vinaweza kuwa vimechangia kuwakurupusha mabosi wa Yanga na kuona wanapaswa kuchukua hatua za haraka, kabla ya wapinzani wao hawajachanganya zaidi.


