MANCHESTER, Uingereza
BAADA ya kuanza msimu huu kwa mwendo usioridhisha, tayari mabosi wa Manchester United wameanza kuelekeza akili zao kwenye soko la usajili wa dirisha dogo la Januari, 2027.
Miongoni mwa nyota walio kwenye rada zao ni mpachikaji mabao tishio wa Crystal Palace, Jean-Philippe Mateta. Mtandao wa talkSPORT umeeleza kuwa Palace wako tayari kumwachia baada ya Mfaransa huyo kutokuonesha nia ya kusaini mkataba mpya.
Usajili wa Mateta una maana gani? Kocha wa Man United, Michael Carrick, anaumiza kichwa kuziba pengo la straika wake, Benjamin Sesko, ambaye hapatikani uwanjani kutokana na majeraha.
Mateta amethibitisha uwezo wake wa kucheka na nyavu kwani ameshafunga mabao 62 na kutoa ‘asisti’ 14 katika mechi zaidi ya 200 alizocheza akiwa na ‘uzi’ wa Palace. Kati ya mabao hayo, 50 amefunga kwenye Ligi.
Nyota mwingine aliye kwenye rada za mabosi wa Man United kuelekea Januari ni mshambuliaji wa Bournemouth, Marcus Tavernier.
Tavernier ni miongoni mwa wachezaji wachache tegemeo kwa Bournemouth kwani ameshacheza mechi zaidi ya 130 tangu aliposajiliwa mwaka 2022 akitokea Middlesbrough.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 amekuwa akicheza vizuri winga ya kushoto, eneo ambalo Man United wanapata nalo shida kutokana na kusuasua kwa kiwango cha Marcus Rashford.
Wakati huo huo, Man United inampigia hesabu kali beki wa kushoto wa Crystal Palace, Tyrick Mitchell. Carrick hakusajili mchezaji mpya kwenye eneo hilo wakati wa dirisha kubwa la kiangazi.
Kwa sasa, Luke Shaw na Patrick Dorgu ni majeruhi. Mitchell, ambaye mkataba wake na Palace utakwisha mwishoni mwa msimu huu, ameshacheza mechi zaidi ya 210, hivyo ana uzoefu mkubwa.


